Polisi yataka wanahabari waheshimu mipaka

DAR-ES-SALAAM : JESHI la Polisi limewataka wanahabari watambue na kuheshimu mipaka katika utekelezaji wa majukumu yao wakati wa Uchaguzi Mkuu.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime alisema hayo Dar es Salaam jana wakati akiwasilisha mada kuhusu wajibu wa waandishi na Jeshi la Polisi wakati wa Uchaguzi Mkuu. Misime aliwasilisha mada hiyo wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari na wadau wengine wakiwemo maofisa wa polisi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu.
Alisema uchaguzi ni kipindi muhimu katika nchi yoyote ile na wananchi wanashiriki ili kutimiza haki yao ya msingi ya kuchaguliwa au kuchagua viongozi. Misime amesema wakati wa mchakato wa uchaguzi polisi na waandishi wa habari kila mmoja ana wajibu ma majukumu yake hivyo ni vyema wote watambue na kuheshimu mipaka wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
Alisema waandishi wa habari wana jukumu na mchango mkubwa kipindi cha uchaguzi, hivyo watekeleze wajibu kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu, weledi na kutokutanguliza masilahi binafsi. SOMA: Maofisa Waandamizi Jeshi la Polisi wajipanga kuimarisha amani
Misime alisema pia ni wajibu wa waandishi kuzingatia weledi, maadili na miiko ya uandishi wa habari, kutoa taarifa sahihi, zenye uwazi na usawa, kuwa mstari wa mbele kutunza na kuhamasisha amani, utulivu na usalama wakati wa uchaguzi.
Alihimiza vyombo vya habari visiwe chanzo cha kuvuruga amani, vitoe elimu inayohusiana na sheria, kanuni, maadili, haki na wajibu kipindi cha uchaguzi na baada na pia vihamasishe uzalendo, amani, utulivu na usalama.Alisema polisi wana wajibu na jukumu la kulinda amani na utulivu katika kipindi cha uchaguzi kwa kulinda maisha na mali, kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu, kupeleleza na kuhifadhi ushahidi na kukamata.



