Prof. Kabudi: AI si tishio la ajira zenu

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi akizungumza na Menejimenti ya Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN). Kikao hicho pia kilihudhuriwa na wanahabari

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi, amewataka wahabari nchini kuwekeza kwenye matumizi ya teknolojia hususani teknolojia mpya ya Akili Mnemba au Akili Unde ‘Artificial Intelligence (AI)’ kwakuwa ni zana ya kurahisisha, kuboresha utendaji kazi huku akiwatoa hofu kuwa teknolojia hiyo sio tishio kwa ajira zao.

Prof. Kabudi amesema hayo leo akiwa Makao Makuu ya Ofisi za Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Barabara ya Mandela, Tazara Dar es Salaam, alipoanza rasmi ziara ya kutembelea vyombo vya habari nchini tangu kuteuliwa katika nafasi hiyo na Rais Samia Suluhu Hassan Desemba 08, 2024.

“Jukumu letu kubwa Watanzania na Waafrika kuhakikisha tunawekeza kwenye utengenezaji wa maudhui ‘content creation’ mengi kuhusu nchi zetu kwakuwa AI haizalishi taarifa bali huchukua taarifa kutoka vyanzo tofauti,” amesema Prof. Kabudi.

Advertisement

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Asha Dachi akimlaki Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi alipotembelea TSN

Katika hatua nyingine, amewataka wanahabari nchini kutabahari katika tasnia yao, kujikita katika kujenga uelewa, na kuondokana na tabia za uvivu kwani tasnia hiyo ni muhimu katika kuikosoa jamii, kuijenga, kutunza utamaduni, kutangaza mambo mazuri ya nchi na serikali pia kuionesha fursa mbalimbali kwaajili ya maendeleo yao na taifa kwa ujumla.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi alipotembelea chumba cha habari cha Gazeti la Daily News

“Tunahitaji waandishi wa aina hiyo, wanaoandika kwa maki na uketo. Kama kuna eneo linalohitaji ubunifu wa hali ya juu ni sekta ya habari kwakuwa teknolojia inabadilika kila uchwao,” amesema Waziri Kabudi akielezea umuhimu wa wanahabari kutabahari ‘specialization’ ili kuwa na habari za kina, zenye tija kwa taifa.

Prof. Kabudi pia amesisitiza uzalendo kama njia bora ya kudumisha umoja kwa kusema kuwa uzalendo ni kuipenda nchi yako, kuilinda, kuienzi na kuthamini tunu zake kama umoja, amani na upendo.

SOMA: UTEUZI: Kabudi apewa Wizara ya Michezo, Silaa Mawasiliano