MTAALAMU wa uchumi ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Humphrey Moshi amesema kuchomoza kwa mataifa ya Afrika Mashariki katika orodha ya matajiri barani Afrika ni ishara kuwa uchumi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) unakua.
Profesa Moshi aliyasema hayo alipozungumza na HabariLEO Afrika Mashariki na kusisitiza kuwa, ni kwa kawaida uchumi unapokua, huenda sambamba na watu wa kipato fulani ambao nao huchangia katika ukuaji huo.
Ripoti mpya ya utajiri iliyotolewa na Kampuni ya Utafiti ya New World Wealth and Henley & Partners iliyotolewa hivi karibuni ilionesha Kenya inaongoza katika mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika nafasi ya tano barani Afrika.
Alisema kupitia matajiri, wananchi hupata fursa ya kupata ajira kwa kuwa uwekezaji unaofanywa na matajiri hao huhitaji nguvukazi ambayo ni wananchi.
Alisema mfano bora wa watu wa namna hiyo, ni mfanyabiashara, Said Salim Bakhresa ambaye amechangia kwa kiasi kikubwa kuzalisha nafasi za ajira nchini.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Utafiti ya New World Wealth and Henley & Partners, Kenya inaongoza katika EAC katika nafasi ya tano barani Afrika ikifuatiwa na Tanzania inayoshika nafasi ya saba katika orodha hiyo inayoongozwa na Afrika Kusini.
Mataifa mengine ya EAC ni Uganda inayoshika nafasi ya 12 huku Rwanda ikishika nafasi ya 17 kati ya mataifa 54 ya Afrika.
Kwa mujibu wa Profesa Moshi, mataifa tajiri ya Afrika Mashariki yanapaswa kujikita kusaidia jamii kwani ni aibu kwa tajiri kujifungia ndani na kupata huduma zote huku nje ya nyumba yake kukiwa na watu wasio na huduma muhimu katika maisha kama maji, chakula na malazi.
Ripoti hiyo inayochambua namna utajiri wa watu binafsi unavyochangia ukuaji wa uchumi wa nchi na kanda husika, imeonesha Jiji la Nairobi mbali na kuchangia pakubwa katika ukuaji wa uchumi wa Kenya, lina watu 5,000 ambao utajiri wao unafika Dola za Marekani milioni moja sawa na takribani Sh bilioni 2.34 za Tanzania.
Jiji la kibiashara la Dar es Salaam lililoshika nafasi ya 12 ndilo lililoipaisha Tanzania kutokana na kuwa na shughuli nyingi za kibiashara likielezwa kuwa na watu 1,300 wenye ukwasi unaofikia Dola za Marekani 790,000 sawa na takribani Sh bilioni 1.82 za Tanzania.
Kwa mujibu wa ripoti, majiji mengine ya EAC ni Kampala nchini Uganda lenye matajiri 900 wenye ukwasi unaofika bilioni 1.5 huku Jiji la Kigali nchini Rwanda likiwa na matajiri wanaofika 500 na ukwasi wao ukiwa ni sawa na takribani Sh bilioni 1.3 za Tanzania.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Henley & Partners, Juerg Steffen, alibainisha katika ripoti hiyo ya hivi karibuni kuwa, miji 14 kati ya 20 tajiri zaidi duniani iko katika nchi zinazoandaa programu rasmi za uwekezaji, na kuhimiza kikamilifu uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni kama malipo ya makazi au uraia.
Profesa Moshi alizishauri nchi za Afrika Mashariki kujikita katika kilimo cha umwagiliaji kwa sababu ndicho kinachoweza kutengeneza mabilionea katika muda mfupi hali itakayotatua uhaba wa chakula katika nchi wanachama wa EAC.
Taifa linaloongoza kwa kuwa na matajiri wengi kwa mujibu wa ripoti hiyo ni Afrika Kusini kupitia majiji yake ya Johannesburg lenye matajiri 15,200 na Cape Town lenye matajiri 6,800.
Misri inashika nafasi ya pili kupitia Jiji la Cairo lenye matajiri 7,800 na Nigeria ikishika nafasi ya tatu kupitia Jiji la Lagos lenye matajiri 6,300.
Majiji yaliyoongoza duniani na idadi ya matajiri wake katika mabano ni New York, Marekani (345,600); Tokyo, Japan (304,900) na San Francisco, Califonia (276,400).