Rais Mwinyi kuwachukulia hatua viongozi wazembe SNR

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi amesema baadhi ya viongozi wa umma wasiotaka kutatua changamoto wanazowasilishiwa na mfumo wa Sema Na Rais (SNR) kwa kutoona umuhimu watachukuliwa hatua.

Dk Mwinyi amesema hayo leo Machi 29, 2023 akiwa kwenye kikao kazi cha maadhimisho ya miaka miwili ya kuasisiwa kwa kitengo cha Sema na Rais Mwinyi (SNR) kilichopo chini ya Ofisi ya Rais Ikulu.

Rais Dk Mwinyi amebainisha kupitia mfumo huo kuna utambuzi wa kitakwimu kujua kiongozi au taasisi zisizofanya vizuri na sasa wakati umefika kila mmoja aone umuhimu wa kuwajibika.

Akizungumzia mafanikio ya mfumo wa SNR kwa kipindi hicho, Rais Dk Mwinyi amesema mfumo huo umeleta tija kwa wananchi ambao changamoto zao zimetatuliwa kwa kiasi kikubwa na mfumo ataendelea kuusimamia vema.

Alizungumzia pia suala la taarifa za ubadhirifu wa mali za umma na akaonya asitokee kiongozi yoyote kuwatisha wanaowasilisha kero au changamoto kupitia mfumo huo na akaahidi hatua zitachukuliwa dhidi ya kiongozi huyo. Ameahidi mtoa taarifa atalindwa na kuwaambia maafisa wa SNR wafanye kazi zao bila woga.

Habari Zifananazo

Back to top button