RAIS Samia Suluhu Hassan ameshauri nchi za Afrika kuwa na umoja, mshikamano na kudumisha ushirikiano wa serikali zao ili kukabiliana na changamoto zinazowakabili.
Aidha, amempongeza Rais mpya wa Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah kuwa Rais wa pili mwanamke Afrika aliyeko madarakani.
Ameeleza hayo jijini Windhoek nchini Namibia alipozungumza katika uapisho wa Rais Ndaitwah baada ya kualikwa kuwa mgeni rasmi kwenye hafla hiyo.
Rais Samia alisema Afrika inakabiliwa na matatizo mengi ikiwamo umasikini uliokithiri, njaa na ukosefu wa usalama hivyo mshikamano ni msingi wa kufanikisha makabiliano dhidi ya changamoto hizo.
“Kwa mtazamo wangu, mshikamano maana yake ni kuimarisha uhusiano na kudumisha ushirikiano wa karibu kati ya serikali zetu, kama Waafrika, lazima tusimame imara kulindana kama ndugu na kuwa walinzi wa kila mmoja wetu,” alisema Rais Samia.
Changamoto zingine ambazo alisema nchi za Afrika zinapaswa kuzikabili kwa umoja ni kukosa uwiano wa kibiashara, ukosefu wa usalama na madeni.
“Uchumi wetu umeelemewa na madeni, ukosefu wa uwiano wa kibiashara, huku idadi ya watu ikiongezeka na mifumo ya ikolojia ikizidi kupungua. Mipaka yetu si salama kama ilivyokuwa hapo zamani na dhana ya ujirani mwema inapungua kwa kuongezeka kwa migogoro ya ndani,” alisema Rais Samia.
Aliongeza: “Tunapaswa kuhakikisha kuna ukuaji wa uchumi jumuishi na kujitahidi kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu na kujenga Afrika tunayoitaka”.
Akimzungumzia, Rais Ndaitwah alimpongeza kwa kuandika historia na kuongeza hadhi ya juu kwa mtoto wa kike nchini Namibia na Afrika kwa ujumla na kwamba ushindi wake ni fahari kwa Afrika na Watanzania.
“Tanzania unatambulika kama Mama Swapo, jina ulilopewa na Baba wa Taifa letu, Mwalimu Julius Nyerere. Watanzania tuna furaha kuona binti tuliyemlea kwa upendo, sasa ameshika ofisi ya juu kabisa ya uongozi katika nchi hii,” alisema Rais Samia.
Aliongeza kuwa Tanzania na Namibia zimekuwa zikifanya kazi kwa karibu katika maeneo yote ya maendeleo na
kudumisha mshikamano kupitia Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa (UN) na kuwa mshikamano huo utaendelea kudumishwa.
“Katika historia, nchi zetu zimekuwa mstari wa mbele kuendeleza usawa wa kijinsia na maendeleo ya kiuchumi kwa wanawake. Mama Getrude Mongella alikuwa Katibu Mkuu katika mkutano wa kihistoria wa Beijing mwaka 1995, huku Ripota Mkuu wa mkutano huo akiwa Rais Ndaitwah. Si jambo la kushangaza kuwa miaka 30 baadaye, mataifa haya yamedhihirisha juhudi zao kwa kuwa na wanawake katika nafasi ya juu ya uongozi,” alieleza Rais Samia.
Vilevile, alisema tukio hilo la uapisho linapaswa kuwa ukumbusho wa nguvu iliyotumika na waasisi wa mataifa hayo mawili katika kupambania haki na usawa.
Rais Ndaitwah aliyekuwa Makamu wa Rais wa Namibia alishinda uchaguzi kwa zaidi ya asilimia 57 katika uchaguzi uliofanyika Novemba mwaka jana. Rais mstaafu Nangolo Mbumba (83) alikabidhi madaraka kwa Nandi-Ndaitwah katika hafla hiyo iliyosherehekewa kwa kuadhimisha miaka 35 ya Uhuru wa Namibia.
Shangwe na vigelegele vilisikika kwa nguvu wakati, Nandi-Ndaitwah anayejulikana kwa kifupi kama NNN,
alipoapishwa rasmi.
Katika hotuba yake baada ya kiapo, Nandi-Ndaitwah alikiri kuwa kuchaguliwa kwake kunaingia katika historia ya
Namibia huku akisisitiza kuwa wananchi wamemchagua kwa sababu ya uwezo na sifa zake.
Aliongeza kuwa ingawa nchi hiyo imepiga hatua tangu uhuru, bado kuna mengi ya kufanya, ikiwamo suala la ajira.