Rais Samia ahadharisha vijana utajiri wa haraka

 RAIS Samia Suluhu Hassan ameagiza vijana wawe na fikra za mageuzi ya kiuchumi kwa kubuni na kuanzisha miradi badala ya kusubiri kuajiriwa au kutaka utajiri wa haraka.

Alisema hayo jana Paje kisiwani Unguja Zanzibar wakati wa kuhitimisha matembezi ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kuadhimisha miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Rais Samia alisema Mapinduzi ya Zanzibar yalileta ukombozi wa kisiasa hivyo sasa taifa linahitaji ukombozi wa kiuchumi na ustawi wa jamii.

Advertisement

“Nataka kuwaambia kazi ya serikali si kutengeneza ajira, ni kuweka mazingira mazuri ili vijana myatumie kutengeneza ajira. Na hiyo kazi tunaifanya vya kutosha. Naomba muende mkatengeneze ajira kwa mazingira yaliyopo,” alisema.

Alisema zipo fursa katika sekta za kilimo na uchumi wa buluu hivyo vijana wazichangamkie kwa kuwa serikali imeweka bajeti ya kutosha kwenye sekta za uzalishaji ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na nchi ipate maendeleo endelevu.

“Vijana wa leo tunakimbilia kwenye kutaka utajiri. Uwe na nyumba nzuri, uwe na gari zuri, mambo yako yaende hivyo lakini baada ya muda utajiri ule unakugeuka unakupiga. Kama ni jumba zuri huwezi tena kulitunza, kama ni gari huwezi kulitunza unarudi tena kwenye unyonge,” alisema na kuongeza:

“Tunalotakiwa kufanya vijana ni kutengeneza ukwasi, upatikanaji wa fedha, kila muda, kila mara, kila wakati. Muwe na miradi midogo midogo. Kazi ya serikali ni kufanya makusanyo makubwa, vijana nendeni kajitumeni,” alisema.

Alisema serikali imetenga fedha kwa ajili ya wanaoanzisha miradi ya maendeleo ambayo itawasaidia kuvuna fedha na kuinua uchumi wa chini.

“Katika dhana ya uchumi wa buluu wanawake hapa Zanzibar wamefanikiwa kwa kuanzisha mradi wa mwani ambao unafanya vizuri lakini naamini vijana wangeweza kufanya miradi mingi zaidi na kuacha kufanya miradi ya kufanana kwa sababu rasilimali za bahari zipo,” alisema Rais Samia.

Pia alisema uvuvi wa vizimba ni fursa nyingine ambayo vijana wanaweza kuitumia kwani wapo wataalamu wa kutosha na kwamba wanaweza kuuza mazao ya samaki kwenye hoteli na kwa wananchi hivyo kujipatia kipato.

Alisema nchi inaelekea kwenye upungufu wa chakula hivyo vijana wana nafasi ya kuanzisha miradi ya kukabili tatizo hilo kwa kuanzisha miradi ya kuzalisha nyama, mbogamboga na chakula.

Alisema utayari wa vijana kujiajiri utasaidia kupunguza kelele za ukosefu wa ajira kwa kuwa soko la mahitaji lipo hivyo wanaweza kutengeneza uchumi ngazi ya chini na serikali itaendelea na miradi mikubwa ya maendeleo.