Rais Samia anastahili pongezi mageuzi mashirika ya umma

KATIKA moja ya eneo ambalo Rais Samia Suluhu Hassan ameweka mkazo ni kuhusu taasisi za umma na mashirika ya umma kuwa yenye ufanisi na kutoa mchango unaostahili katika kusaidia kuchangia maendeleo ya kiuchumi nchini.

Rais Samia amekuwa akisisitiza kwamba mashirika ya umma yanapaswa kuendeshwa kibiashara na kutoa tija inayokusudiwa kwa serikali, ikiwamo kuchangia katika Mfuko Mkuu wa Serikali na pia kuendeshwa kwa ufanisi na  uwazi.

Ni kwa msingi huo, Rais Samia amekuwa kinara wa kuongoza mageuzi hayo ndani ya taasisi na mashirika ya umma na ndiyo maana chini ya usimamizi wa Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, ofisi hiyo imebeba maono ya Rais kupitia Falsafa ya 4R kwa kubeba mbili kati ya hizo yaani Mageuzi na Kujenga upya.

Katika hilo, matunda yamejitokeza katika uendeshaji wa mashirika hayo na mojawapo ya karibuni ni ongezeko la mapato ya Msajili wa Hazina kwa asilimia 40, na zaidi michango ya mashirika hayo kwa serikali sasa imefikia takribani Sh trilioni moja.

Kwa mujibu wa Mchechu, hadi sasa mashirika hayo yameshakusanya michango ya Sh bilioni 900 kutoka Sh bilioni 500 kipindi kama hiki mwaka jana, na inatarajiwa kuwa kufikia Siku ya Gawio Juni 10, michango itafikia zaidi ya Sh trilioni moja.

Takwimu zinaonesha kuwa mwaka jana Rais Samia alipokea gawio la Sh bilioni 637 kutoka kwenye mashirika na taasisi za umma 145 kati ya 304 zinazochangia asilimia 15 ya mapato ghafi na zile ambazo serikali ina hisa.

Kadhalika kwa miezi 11 mwaka huu, kiasi kilichokusanywa na mapato yasiyo ya kikodi ni sawa na ongezeko la asilimia 15.3 ya makusanyo yote ya mwaka wa fedha 2023/2024 ambayo ni Sh bilioni 767.

Haya ni mafanikio makubwa ambayo yanaakisi maono ya Rais Samia ya kutaka kuwapo kwa mageuzi katika uendeshaji wa mashirika haya ya umma ambayo ni sehemu ya rasilimali kubwa za taifa zinazopaswa kuchangia maendeleo ya nchi.

Tumefurahishwa na mafanikio haya ambayo chachu yake ni maono ya Rais Samia, lakini yakipewa nguvu na usimamizi thabiti wa Ofisi ya Msajili wa Hazina chini ya Mchechu, ambayo yanaonesha kuwa mageuzi haya yameanza kulipa.

Chini ya Mchechu na watendaji wake, tunaamini taasisi na mashirika ya umma yana uwezo wa kuendelea kufanya vizuri zaidi na kuwa na sehemu kubwa ya mchango katika Pato la Taifa kwani takwimu za sasa zinaonesha mbele kuna mwanga zaidi.

Kwa msingi huo, tunapoelekea kwenye Siku ya Gawio wiki ijayo, bodi na menejimenti za taasisi na mashirika haya yapatayo 252 hazina budi kujitathmini kila moja na kuona ni kwa kiasi gani zimetekeleza kwa vitendo maono ya Rais Samia ya kuwa chachu ya kuchangia uimara wa uchumi, badala ya kuwa mzigo kwa serikali.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button