DAR ES SALAAM: RAIS, Samia Suluhu Hassan amewataka washiriki wa Kongamano pili la Wanawake katika Biashara ndani ya eneo huru la biashara barani Afrika kujadili namna ya kuwezesha ushiriki imara wa wanawake katika biashara ndani ya Bara la Afrika.
Akitoa maagizo hayo ya Rais leo Desemba 6, 2023 jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema ni muhimu washiriki wa kongamano hilo kuja na mipango mahsusi ya hatua zinazotakiwa kuchukuliwa na kuimarisha ushirikiano kwa lengo la kuwa na ushiriki wenye tija kwa wanawake katika biashara unakamilishwa.
Majaliwa amesema kufanyika kwa kongamano hilo kwa mara ya pili hapa nchini ni ishara tosha ya kuonyesha dhamira ya nchi kwa washiriki wa eneo huru la biashara barani Afrika kukuza ushiriki wa wanawake katika biashara.
“Kufanyika kwa makongamano haya kunatoa nafasi muhimu kwa wadau mbalimbali kuwawezesha wanawake kujadiliana na kutafuta ufumbuzi wa pamoja wa changamoto zinazokwamisha jitihada za wanawake katika biashara,” amesema.
Amesema kuwa, miongoni mwa faida za kuwa na eneo huru la biashara la barani Afrika ni kusaidia kuongezeka kwa biashara baina ya nchi za Afrika kutokana na nchi kuondoleana ushuru wa forodha.
“Faida nyingine ni kushughulikia kwa pamoja vikwazo vya biashara visivyo vya kodi na kukuza uongezaji thamani wa malighafi zinazozalishwa ndani ya Afrika.
”
Aidha, Majaliwa amesema kuwa, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imeanzisha mfumo rahisi wa biashara (Simplified Trade Regime-STR) kwa ajili ya mauzo ya nje ya mipakani kwa ajili ya kuwasaidia wafanyabiashara wadogo kwa mipakani.
Amesema, uamuzi wa kuazisha mfumo umeonesha dhamira ya jumuiya hiyo katika kutambua ushiriki mkubwa wa wanawake kwenye biashara ndogo ndogo za mipakani.
Naye Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji amesema kampuni nane za Kitanzania zimeanza kufanya biashara na zimepeleka biashara mara 17 kwenye nchi tano zilizopo katika ndani ya eneo huru la biashara barani Afrika.
Kwa upande wake, Waziri wa Menendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Doroth Gwajima amesema, uwezeshaji wanawake na vijana kiuchumi ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ili kuleta usawa wa kijinsia na hivyo kufikia maendeleo jumuishi na endelevu.
“Katika kufikia adhma hiyo serikali imeridhia na inatekeleza mkataba na maazimio ya kikanda na kimataifa ikiwemo mkataba wa eneo huru barani Afrika ambao unatoa fursa za kiuchumi kwa wanawake na hata wanaume ndani ya bara letu,”amesema Gwajima