MKUU wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella ameahidi kuwezesha upatikanaji wa bima za afya kwa watoto 144 wanaoishi katika kituo cha kulelea watoto waliotoka mazingira magumu cha Moyo wa Huruma mjini Geita.
Shigella ametoa ahadi hiyo wakati akikabidhi zawadi Rais Dk Samia Suluhu kwa watoto wa Kituo cha Moyo wa Huruma ikiwa ni sehemu ya faraja katika kusherehekea Mwaka Mpya 2025.
Amesema bima kwa watoto hao ni sehemu ya kutambua mchango wa viongozi wa dini na taasisi za kidini zinazoendelea kujitoa kwa ajili ya kusimamia maadili ya watoto na jamii na kuwalinda watoto.
“Niwashukuru viongozi wa dini, kwa kuendelea kuiunga mkono serikali yetu, maana bila viongozi wa dini, maadili yetu kama taifa huenda tukafika mahala likazidiwa, kwani hatuwezi kuwa na polisi kila mahala.
“Hatuwezi kuwa na magereza kila mahala, kwa hiyo kupitia viongozi wa dini watanzania ambao wanakengeuka viongozi wa dini wanatusaidia kuwarudisha kwenye misingi inayotakiwa” amesema.
Ametaja miongoni mwa zawadi za Rais Dk Samia kwenye kituo hicho cha watoto cha Moyo wa Huruma ni mchele kilo 100, sukari kilo 40, unga wa ngano kilo 50, mbuzi wawili pamoja na vinywaji.
Msimamizi wa Kituo cha Moyo wa Huruma, Sister Marie Launda amemshukuru Rais Dk Samia kwa msaada huo pamoja na mkuu wa mkoa kwa ahadi ya bima za afya kwa watoto kwani itapunguza gharama za matibabu.
“Tunachoangalia ni kwamba gharama za matibabu zipo juu sana kwa sasa, kwa hiyo bima ni muhimu kuhakikisha mtoto akiugua anapata anapata matibabu stahiki” amesema Sister Marie.