Rais Stubb aeleza siri Finland kuongoza kwa furaha duniani

RAIS wa Jamhuri ya Finland, Alexander Stubb ametoa siri ya nchi hiyo kuwa taifa lenye furaha zaidi duniani kwa miaka 17 mfululizo inatokana na wao kupenda misitu, uoto wa asili na kuwa asilimia 70 ya taifa hilo limezungukwa na vitu hivyo pamoja na maziwa ya asili zaidi ya 1,000.
Rais Stubb amesema hayo Dar es Salaam wakati akizindua Mradi wa Kusimamia Uhifadhi wa Misitu, Matumizi Bora ya Ardhi na Kuongeza Thamani ya Mazao ya Misitu (FORLAND), wenye thamani ya Euro milioni 20.
Mradi huo unalenga kukuza kanuni endelevu za uhifadhi wa misitu, kuboresha maisha ya wananchi, kuimarisha ukuaji wa uchumi wa Tanzania pamoja na kuendeleza usimamizi wa misitu katika jamii, upandaji miti na maendeleo ya mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanywa kwenye Bustani ya Botanical, Dar es Salaam, Rais Stubb pia alishiriki upandaji miti na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Tanzania na Finland katika sekta ya misitu.
“Nina imani mti nilioupanda utakua kama ulivyo ushirikiano kati ya nchi zetu katika sekta ya misitu, hususani kupitia mradi huu wa Forland,” alisema.
Rais Stubb alisema Finland ina misitu inayochukua asilimia 70 ya eneo la nchi hiyo na kwamba bidhaa zake za misitu zinatambulika kwa ubora na uimara wake.
“Tunapokuwa na uzalishaji endelevu wa mazao ya misitu ambazo ni pamoja na bidhaa tunazozipenda kwetu, inakuwa na maana kubwa sana na ndiyo maana sisi tumeenda mbali tumeanza kujenga nyumba kwa kutumia mbao ambazo zinadumu kwa muda mrefu ukilinganisha na saruji,” alisema Rais Stubb.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Furaha Duniani ya mwaka 2025, nchi 10 zinazoongoza kwa furaha duniani ya kwanza ni Finland ikifuatiwa na Denmark, Iceland, Sweden, Uholanzi, Costa Rica, Norway, Israel, Luxembourg na Mexico.
Ripoti hiyo inasema nchi hizo zimepata alama za juu kutokana na viashiria vya ustawi ikiwa ni pamoja na msaada wa kijamii, uhuru wa kufanya uamuzi, mapato, afya, ukosefu wa rushwa na ukarimu.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk Pindi Chana alisema mradi wa FORLAND unatekelezwa katika mikoa ya Kusini mwa Tanzania, ukiwa na lengo la kuimarisha usimamizi wa rasilimali za misitu na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika jamii zinazozunguka misitu hiyo.
“Nchi yako (Finland) imekuwa mshirika muhimu kwa Tanzania katika sekta ya misitu ikiwa imesaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali,” alisema.
Alitaja mipango hiyo ni, Mpango wa Usimamizi wa Eneo la Hifadhi ya Usambara Mashariki (1988–2002), vyuo vya misitu nchini Malawi, Tanzania na Zambia (1999– 2005), Programu ya Kitaifa ya Misitu (2005–2010) na Biashara ya Kibinafsi ya Misitu na Kaboni (2010–2011).
Alisema Finland pia, imeisaidia Tanzania kupitia Programu za Kitaifa za Misitu na Nyuki (2013–2016) pamoja na Ufuatiliaji na Tathmini ya Rasilimali za Misitu (Naforma) tangu 2009.