RC amtaka Mhandisi kuhamishia ofisi kijijini

IRINGA: MKUU wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba amemtaka Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Nicco Kasililika kuondoka ofisini kwake na kupiga kambi katika kijiji cha Mlenge, Pawaga, zaidi ya kilometa 100, ili kusimamia ujenzi wa kituo cha afya alichoagiza kiwe kimekamilika ifikapo Juni 15, mwaka huu.

Hatua hiyo imekuja baada ya mhandisi huyo pamoja na viongozi wengine wa halmashauri hiyo kutoa taarifa inayoonesha uwezekano wa kituo hicho kukamilika kabla ya muda huo kuonekana ni mdogo.

“Mhandisi kuanzia kesho sitaki kukuona au kusikia upo ofisini kwako. Nakutaka uende Pawaga wewe mwenyewe ukasimamie ujenzi huo ili wananchi waanze kupata huduma,” alisema wakati wa ufunguzi wa baraza la madiwani wa halmashauri hiyo lililofanyika mjini Iringa leo.

Advertisement

Akijibu swali la Mkuu wa Mkoa aliyetaka kujua ni mara ngapi ameenda kukagua kituo hicho tangu atoe agizo la kukamilisha ujenzi wake mwezi mmoja uliopota, Kasililika alisema; “Nimekwenda kule kama mara nne tu mkuu lakini msaidizi wangu yupo huko siku zote.”

Akizungumzia maendeleo ya ujenzi huo, Kasililika alisema unaendelea kwa kasi kubwa ukiwa tayari umefikia kiwango cha lenta na kwamba wakati wowote kuanzia sasa kenchi zitapigwa, tayari kwa ajili ya kuezeka.

Mkuu Mkoa alisema yapo mambo katika uongozi wake anaweza kuyavumilia lakini sio ucheleweshaji wa miradi ambao kwa halmashauri hiyo ni kama tatizo sugu.

“Kiukweli moja ya halmashauri yenye pesa nyingi za miradi ni pamoja na halmashauri yenu ya Iringa lakini chakushangaza ipo nyuma sana katika kutekeleza miradi,” alisema.

Alimpongeza mbunge wa Isimani William Lukuvi na mbunge wa Kalenga Jackson Kiswaga akisema wanapambana sana kuhakikisha halmashauri hiyo inayounda majimbo hiyo inapata fedha nyingi za miradi.