MKUU wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi wa Umeme Vijijini (REA) awamu ya tatu mzunguko wa pili Mkoa wa Kagera kuharakisha mchakato wa utekelezaji kwa muda aliongezewa, ili kuwasaidia wananchi wa vijijini kupata umeme haraka.
Mkutano wa kufuatulia hali ya utekelezaji wa Mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili mkoani Kagera, umefanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, ambapo viongozi na watendaji mbalimbali kutoka REA, TANESCO, wabunge wa Mkoa wa Kagera walikaa pamoja na kuzungumzia hali ya mradi na utekelezaji wake.
Mkandarasi anayetekeleza mradi huo Kampuni ya JV alipaswa kumaliza Januari 30 mwaka 2023, lakini ameongezewa muda mpaka April 2023 kukamilisha kazi yake.
“Wakandarasi badilisheni tabia zenu za kuwa mnataka kuongezewa muda, unavyoenda kuomba tenda serikalini unakuwa unaelewa uwezo wako wa kifedha timu uliyonayo utendaji kazi wako, usisubiri upate tenda ndo uanze kusema unajua nilikuwa sina wafanyakazi ?
“Wananchi wanachotaka ni kuona umeme unawaka, tumeongeza shule na maabara za sayansi, vituo vya afya tunahitaji umeme mkandarasi usitukwamishe,”alisema Chalamila.
Mkurugenzi wa Uendelezaji Masoko na Teknolojia ambaye alimwakilisha Mkurugenzi wa REA, Mhandisi Advera Mwijage alisema kuwa Mkoa wa Kagera una vijiji 662 Kati ya hivyo mpaka sasa Vijiji 525 vimewashwa umeme.
Alisema kuwa mkandarasi huyo alisaini mkataba wa kuwasha umeme katika vijiji 137 kwa gharama ya shilingi Bilioni 37 na mkataba huo ulisainiwa Julai 9, 2021 ambapo utekelezaji wa mradi ulipaswa kukamilika Januari 30, 2023.
Alisema REA inatambua kuna changamoto ya kupanda kwa vifaa ilijitokeza, lakini wakandarasi wote waliitwa na kuongezewa fedha kwa ajili ya kununua vifaa, ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi.
Meneja msimamizi wa Mradi wa REA mkandarasi kutoka kampuni ya JV, Eva Fumbuka alikiri kuwepo kwa changamoto mbalimbali ambazo zilikwamisha mradi hasa mabadiliko ya upandishwaji bei ya vifaa, Geographia ya mkoa wa Kagera na hali ya hewa.
Alikihakikishia kikao hicho kuwa muda aliopewa atamaliza mradi katika vijiji vyote na wananchi watapata umeme kwa sababu tayari amepata ufumbuzi wa changamoto na ameongeza kikosi kazi cha kutekeleza miradi huo.