RC Singida aagiza viongozi CHAMWAI kuwekwa rumande

MKUU wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda, ameagizwa kuwaweka rumande watu watano waliokuwa viongozi wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Walimu Iramba (CHAMWAI), mpaka atakapowapeleka kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, Januari 31, mwaka huu.

Serukamba ametoa agizo hilo baada ya kusikiliza malalamiko ya walimu wastaafu wasiopungua 100, kwenye ukumbi wa mikutano ofisini kwake na kuelezwa kuwa uanachama wao CHAMWAI ulikoma walipostaafu kazi lakini mpaka sasa hawajalipwa fedha zao, zaidi ya Sh. Milioni 300.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wastaafu hao wanasema wakati Wilaya ya Iramba haijagawanywa kupatikana Wilaya ya Mkalama, waliridhia kukatwa kuanzia Sh 10,000 kwenye mshahara zilizowekwa kwenye chama hicho huku wakikopeshwa fedha ambazo walikuwa wakizirudisha na riba.

“Makubaliano yanasema mwalimu anapostaafu, alipwe haki zake ziwemo hisa lakini mpaka sasa wengine tuna miaka kumi tangu tustaafu hatujalipwa hata kumi,” amesema mmoja wa walimu hao.

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wa Mkoa huo, Mzalendo Madege, amekiri kutambua sakata hilo, kwamba pamoja na mambo mengine chama hicho kilikopeshwa fedha na Benki ya CRDB lakini kuna kasoro katika mchakato wa mkopo huo.

Baadhi ya viongozi na walimu wastaafu wakifuatilia mkutano wa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba. (Picha zote na Editha Majura,Singida).

Serukamba baada ya mahojiano na maofisa wa CRDB, watendaji wa Wilaya za Iramba, Mkalama na wakurugenzi akasema kwa uzoefu wake katika ukaguzi wa hesabu, anaona tatizo hilo ni kubwa kuliko linavyochukuliwa.

“Nawahakikishia kila mmoja atalipwa haki yake, naomba nipitie hizi nyaraka mpaka Jumanne, saa 5 asubuhi mje tujifungie humu, tuhojiane na kila muhusika mpaka kieleweke,” amesema Serukamba.

Amesema licha ya kupambania haki za wastaafu hao, anataka kuhakikisha chama hicho pia kinabakia salama na kinaendelea kunufaisha walengwa bila kuhujumiwa.

Pia viongozi wa chama hicho wa chama wa sasa, mrajisi wa vyama, wakurugenzi wa halmashauri hizo mbili, TAKUKURU, wakuu wa wilaya hizo, usalama wa taifa, maofisa husika wa CRDB nao wametakiwa kutokosa kwenye mkutano huo na wapeleke nyaraka zote zinazohusika.

Amesema kwa haraka amebaini kasoro nyingi, ikiwamo hati ya udhamini wa chama hicho kukopa fedha CRDB, kusainiwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida (hakutaja majina) ilhali chama kipo kwenye halmashauri za Iramba na Mkalama.

Ameagiza mkurugenzi huyo kutokosa kwenye kikao cha Jumanne, ambacho amesema kitafukunyua mgogoro huo, mpaka kiini chake na ufumbuzi upatikane.

“Ijulikane aliyesaini hati ya udhamini ni nani, fedha iliwekwa kwenye akaunti ya nani? Kama ni akaunti binafsi wahusika wabanwe, kama ni akaunti za chama, nani alizitoa?” Amehoji Serukamba.

CRDB nao wametakiwa kuwasilisha nyaraka zote kuhusu mkopo huo bila kukosa muktasari uliosainiwa na watu wote wanaotakiwa kuusaini, vinginevyo benki itabeba gharama.

Naye Mwenda akasema mmoja kati ya waliokuwa viongozi wa chama hicho, alishafariki na kuahidi kuwapeleka waliopo kwenye mkutano huo kama ilivyoelekezwa.

Habari Zifananazo

Back to top button