RC Singida awapa somo MaDC wapya

WAKUU wapya wa Wilaya mne za Mkoa wa Singida, wametambulishwa rasmi kwa viongozi wenzao wa halmashauri zote za mkoa huo na kupewa dondoo kuhusu masuala tofauti katika wilaya zao na matarajio ya Mkuu wa Mkoa huo, Peter Serukamba aliyeongoza tukio hilo.

 

Mkuu mpya wa Wilaya ya Manyoni, Kemilembe Lwota, aliyesimama. (Picha zote na Editha Majura).

Tukio hilo limefanyika leo Februari 7, 2023, ambapo Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Kemilembe Lwota alidokezwa kuwa pamoja na shughuli nyingine anakwenda kukabiliana na zigo la migogoro ya ardhi ambayo inatarajiwa akasaidie kuipatia ufumbuzi, huku Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Moses Machali amedokezwa kuhusu changamoto ya uchafu katika mazingira ambayo inatarajiwa akatumie mbinu mbadala kuipatia ufumbuzi.

Serukamba amemtambulisha Thomas Apson kuwa ndiye Mkuu wa Wilaya ya Ikungi na Joshua Nassari kuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba na kwamba anaamini watashirikiana kuacha alama kwenye mkoa huo, ikiwamo kuadhimisha miaka 60 ya Mkoa huo kuanzishwa itakapotimia Oktoba 15 mwaka huu.

Pamoja na kutakiwa kutekeleza majukumu yao, wakuu wa wilaya wote mkoani humo wametakiwa kutotumia nguvu pasipokuwa na lazima, labda jambo liwe limeshindikana kabisa kwa sababu Serukamba siyo muumini wa mambo hayo, ingawa amekiri kuwapo watu wanaokwaza sana lakini akaomba wawe wavumilivu na watumie njia tofauti kuwezesha mambo kwenda.

 

Mkuu mpya wa Wilaya ya Iramba, Joshua Nassari (aliyesimama).

“Pia kuepuka misuguano na wakurugenzi, msijiingize kwenye michakato ya utekelezaji, waacheni na fedha zao lakini muwadai kinachotakiwa kufanyika, ikiwa ni ujenzi wa shule nyie mdai shule ionekane ingawa mambo yasipokwenda vizuri tutalazimika kuingilia kati,” ameagiza Serukamba.

Alihadharisha kwamba hapendi kudanganywa, hata kama jambo halijakwenda ilivyotarajiwa ni vizuri akaelezwa ukweli ili kwa pamoja watafute ufumbuzi, mtu mzima kumdanganya yeye huitafsiri kuwa ni kumdharau tabia ambayo hana uwezo wa kuivumilia.

Habari Zifananazo