Umeme kusambazwa vitongoji 134 Ruvuma
RUVUMA:SERIKALI kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imetenga shilingi bilioni 14.56 kwa ajili ya kusambaza umeme katika vitongoji 135 vya Mkoa wa Ruvuma, ambapo kaya 4,455 zitanufaika na mradi huo.
Mhandisi Msimamizi wa Miradi ya Umeme REA Kanda ya Kusini, Deogratius Nagu, amebainisha hayo leo wakati wa kumtambulisha mkandarasi aliyeshinda zabuni ya kutekeleza mradi huo, Kampuni ya CCC International Nigeria LTD, mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Ahmed.
Amesema kuwa mradi huo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha maendeleo yanafika kote nchini.
Aidha Kanali Ahmed amesistiza juu ya umuhimu wa mkandarasi kukamilisha mradi huo kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa pamoja na kutoa wito kwa wananchi kushirikiana na mkandarasi na kulinda miundombinu ya umeme itakayowekwa kwenye maeneo yao.
Hata hivyo, Mradi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 24, hadi ifikapo Septemba 2026. Utekelezaji wake unahusisha vitongoji 135 kutoka majimbo tisa ya wilaya za Songea, Mbinga, Nyasa, Namtumbo, na Tunduru.
SOMA :Bil 100/- kupeleka umeme vijijini Kigoma
Kwa sasa, Mkoa wa Ruvuma una jumla ya vijiji 554 ambavyo vyote vimekwishafikishiwa umeme, na kazi inayoendelea ni kuhakikisha umeme unafika vitongojini kwa asilimia kubwa zaidi.