REA yaanza kusambaza mitungi ya gesi 13,020 Mkoani Songwe

SONGWE : WAKALA wa Nishati Vijijini (REA), kwa kushirikiana na kampuni ya Oryx Gas Tanzania Limited, imeanza rasmi kusambaza mitungi ya gesi ya kilo 6 kwa wakazi wa mkoa wa Songwe, ambapo wananchi wa wilaya ya Mbozi wameanza kununua mitungi hiyo kwa bei ya ruzuku.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, amewapongeza REA na Oryx kwa kuanzisha mpango huu wa kusambaza nishati safi, akisisitiza umuhimu wa kutoa elimu kuhusu usalama wa gesi ya kupikia na faida ya nishati safi kiafya na kimazingira.

Alisema, Rais Samia Suluhu Hassan ni mhamasishaji mkubwa wa matumizi ya nishati safi, na mikoa ya pembezoni kama Songwe inafaidi sana kutokana na mpango huu.

Advertisement

SOMA: REA kusambaza mitungi ya gesi zaidi ya 19,000 Mbeya

Meneja Mradi wa Nishati Safi, Vencha Maganga, alieleza kuwa serikali kupitia REA imetenga fedha kwa ajili ya kusambaza nishati safi katika maeneo ya vijijini, na aliwataka wananchi kuchangamkia fursa ya kununua mitungi ya gesi kwa bei ya ruzuku ya shilingi 20,000 badala ya bei ya kawaida ya shilingi 40,000.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi, George Msyani, aliwapongeza wananchi kwa kuchangamkia fursa ya kununua mitungi hiyo kwa bei nafuu katika kitongoji cha Mlowo, wilayani Mbozi.

Wilaya zitakazonufaika na usambazaji wa mitungi hiyo ya gesi ni pamoja na Mbozi, Ileje, Momba na Songwe.

 

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *