UJENZI wa nyumba 35 za waathirika wa maporomoko ya udongo na mawe wilayani Hanang mkoani Manyara uliojengwa na Tanzania Red Cross (TRCS) imeelezwa kuwa ni kielelezo cha ubinadamu na utu kwa binadamu wengine.
Ujenzi wa nyumba hizo ni kati ya nyumba 108 zilizokuwa zinajengwa na serikali ambapo Tanzania Red Cross imezijenga.
Rais wa Red Cross, David Kihenzile amekagua na kutembelea nyumba 35 zilizojengwa akiambatana na wajumbe wa bodi katika jitihada za kusaidia serikali za kujenga nyumba 108.
“Mradi huu ni kielelezo duniani kote Red Cross inajenga majengo ya muda kwa mara ya kwanza ndio hapa Tanzania tumejenga makazi ya kudumu hatua ambayo inadhihirisha kukua kwa diplomasia ya nchi na kuaminika,” amesisitiza Kihenzile.
Katibu wa TRCS Lucia Pande amesema ujenzi wa nyumba hizo umepata fedha kutoka International Federation of Red Cross and Red Cresent (IFRC) ambao wamegharamia jumla ya nyumba 33 ambapo nyumba 2 ni kutoka Spanish Red Cross.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Almishi Hazali ameeleza kuwa TRCS imejenga heshima kwa watanzania na kudhihirisha kuwa ni kisaidizi cha serikali kutokana na utoaji wa misaada ya kibinadamu wilayani Hanang kwa kipindi chote na baada ya mafuriko kutokea.