‘Royal Tour’ yazinduliwa Sweden  

Serikali ya Tanzania kupitia ubalozi wake uliopo Sweden imezindua filamu ya Royal Tour jijini Stockholm kwa lengo la kuwavutia watalii kutembelea vivutio mbalimbali hapa nchini.

Sekta ya utalii duniani ilipata pigo miaka ya karibuni baada ya kusambaa kwa Covid-19 lakini sasa Tanzania imekuja na mikakati mbalimbali, ikiwemo filamu ya Royal Tour, kwa lengo la kuichechemua.

Akizungumza kutoka Skockholm Sweden, Balozi wa Tanzania nchini humo, Grace Olotu amesema sherehe za uzinduzi wa  filamu ya Royal Tour mjini Stockholm zilizofanyika hivi karibuni zilihudhuriwa na waandishi wa habari za utalii  nchini humo ambao wanatarajiwa kuitangaza kwa soko la utalii la nchi hiyo.

Amesema uzinduzi wa Filamu hiyo iliyoandaliwa na mtaalam kutoka Marekani akiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inayoelezea  vivutio vya utalii vya Tanzania umefanyika kwa lengo la  kuitangaza ili kuwavutia watalii kutoka nchi tisa za Scandinavia na ukanda wa bahari ya Baltic.

Balozi Olotu amesema Serikali itaendelea na juhudi za kutangaza utalii kwa kuzindua filamu ya Royal Tour katika  nchi zote tisa anazozisimamia ikiwemo Norway, Finland, Denmak, Iceland, Lithuania, Istonia, Latvia, Ukraine na Sweden ambapo tayari uzinduzi huo umefanyika hivi karibuni.

“Nina matumaini makubwa kuwa juhudi za Serikali kupitia ubalozi wetu kwa kushirikiana na wadau wengine zitazaa matunda na kuongeza idadi kubwa ya watalii baada ya kipindi cha mpito ambapo nchi nyingi zilikabiliana na athari za UVIKO 19 katika sekta ya utalii,” amesema Balozi Olotu.

Aidha, Balozi wa hiari wa Utalii wa Tanzania katika nchi hizo,  Hazze Shija Sandström ambaye pia alihudhuria sherehe za uzinduzi huo alisema juhudi zinazoendelea za kuutangaza utalii wa Tanzania duniani zitaongeza watalii nchini mwaka huu na kufungua fursa za utalii katika maeneo ya kusini mwa Tanzania ambayo amesema yana vivutio vizuri kupita eneo lolote la nchi.

“Matumaini yangu ni kuwa Watanzania watakuwa tayari kuwapokea wageni na kuwapa huduma bora kwa ukarimu na uaminifu ili waweze kufurahi, kupeleka taarifa nzuri kuhusu utalii wa Tanzania na kurudi tena nchini “ amesema Sandstrom ambaye pia ni mwekezaji nchini Tanzania katika sekta ya utalii nyanda za juu Kusini.

Akizungumzia Diplomasia ya Uchumi, Balozi Olotu amesema takwimu zinaonyesha nchi hizo zimewekeza kiasi cha dola za kimarekani bilioni 1  katika miradi mbalimbali 193 nchini  ambayo imeajiri takribani Watanzania 12,000.

Ametaja sekta ambazo nchi hizo zimewekeza kuwa ni pamoja na kilimo, utalii, usafirishaji, uzalishaji, maliasili, nishati, ujenzi na mawasiliano.

Amesema Serikali inaendelea kutekeleza sera yake ya Diplomasia ya Uchumi duniani  kwa kutangaza utalii, fursa za biashara na uwekezaji zilizopo  nchini.

Habari Zifananazo

Back to top button