JUMATANO iliyopita, gazeti la HabariLEO chini ya makala yaenye kichwa cha habari, ‘TGNP Imechangia Ustawi wa Demokrasia Tanzania,’ ilimwelezea Mary Rusimbi alivyoshiriki harakati za kutetea usawa wa kijinsia kupitia taasisi mbalimbali alizoongoza ikiwemo ya Mtandao wa Jinsia Tanzania. Katika makala haya, mwandishi STELLA NYEMENOHI anaonesha shuhuda za watu mbalimbali kuhusu namna utendaji wake ulivyowagusa. ENDELEA…
‘Rusimbi alinijenga’
MARY Rusimbi ni miongoni mwa waanzilishi wa Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT) mwaka 2018.
“Mimi na watu wawili, watatu tulianzisha mfuko,” anasema na kuongrza kuwa, alikuwa mkurugenzi mtendaji wa kwanza wa mfuko huo unaotoa fedha kuunga mkono shughuli za maendeleo ya wanawake.
“Ukisikia tumesapoti wanaume ujue kuna ajenda ya kusapoti wanawake,” anaeleza na kuainisha maeneo ikiwamo yanayohimiza ushiriki wa wanawake katika siasa. Aliondoka WFT 2022 na sasa ni Mwenyekiti wa Bodi.
Mratibu wa Taifa wa taasisi inayojihusisha na masuala ya kitaifa ya wanawake ya Women Crossp Party Platform, Dk AveMaria Semakafu ana ushuhuda juu ya utendakazi wa Rusimbi na alivyonufaika na WFT.
Anasema alimfahamu Rusimbi tangu akiwa katika Ubalozi wa Uholanzi nchini Tanzania katika kipindi cha maandalizi ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Wanawake wa uliofanyika Beijing, China 1995.
Kwa mujibu wa Dk Semakafu, Rusimbi alitoa hamasa na malezi kwa wanaharakati vijana.
Anasema akiwa na umri wa miaka 32, Rusimbi alimjenga hadi kufikia hatua ya kuteuliwa kuwa katibu mwandaaji wa ushiriki wa asasi za kiraia Beijing chini ya Umoja wa Asasi Zisizo za Kiserikali (TANGO).
Kwa mujibu wa Semakafu, walipeleka wanawake 383 Beijing. Anasema licha ya Rusimbi kuwa ofisa mwandamizi ubalozini, alishiriki kikamilifu katika maandalizi kama Mtanzania wa kawaida.
Taasisi ya ULINGO (Umoja wa Vyama vya Wanawake Wanasiasa Tanzania) ni zao la uwezeshaji wa Rusimbi na Dk Fenella Mukangara waliowezesha wanawake viongozi wa jumuiya kuachana na jazba za kichama na kuunda taasisi hiyo.
Aidha, wakati wa mchakato wa katiba mpya kwa mujibu wa Semakafu, Rusimbi alijenga nguvu na sauti ya pamoja; kipindi hicho akiwa Mkurugenzi wa WFT.
Semakafu anasema: “Aliongoza NGOs (asasi zisizo za kiserikali) na CBOs (taasisi za kijamii) zaidi ya 200 kwenye kudai ajenda ya mwanamke.”
Anasema mkakati huo uliwezesha kuundwa Mtandao wa Wanawake na Katiba ambao umekuwa chachu ya kuibuka mitandao mingine mingi nchini.
Uliwezesha wanawake kubaki na ajenda mtambuka zilizowezesha kupokewa kwa madai 11 kati ya 12.
“Kwa mafanikio hayo, tuliendeleza nguvu ya pamoja ambayo imezalisha mtandao wa kupinga rushwa ya ngono na mtandao wa wanawake viongozi Afrika,” anasema Semakafu.
Anamtaja Rusimbi kama kungwi na mkufunzi kwa wanawake, wanaume, vijana na wanaharakati juu ya maana halisi ya harakati kuwa ni kupigania ajenda ipokewe, kupigania mabadiliko ya mtazamo ili kupokea mabadiliko chanya.
Mama wa demokrasia
Mchambuzi wa masuala ya siasa na Mwalimu wa Masuala ya Diplomasia, Kituo cha Mahusiano ya Kimataifa cha Dk Salim Ahmed Salim cha Dar es Salaam, Deus Kibamba anasema Rusimbi ni ‘Mama wa demokrasia kwa vitendo’.
“Rusimbi anayaishi anayosema. Ana moyo wa utajiri…H ivi nilivyo leo, asilimia 90 ni zao la Mama Rusimbi,” anasema Kibamba aliyewahi kuwa Ofisa Mwandamizi wa Sera, Jinsia na Bajeti za Kijinsia wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP Mtandao).
Anamtaja kuwa ni mama anayethamini na kutambua mtu na kazi yake.
“Ni mama asiye na choyo. Ukifanya kazi kubwa utalipwa zaidi… Ukifanya hivyo watu wanakuheshimu na wako tayari kufanya kazi,” anasema Kibamba.
Anasema ni kiongozi asiyetetereka ambaye hata akiambiwa ‘tuhuma’ za mfanyakazi wa chini yake, hakurupuki kuchukua hatua, bali hutafuta ukweli.
Anaeleza zaidi kwamba ni mtu wa staha na subiri anayejitofautisha na viongozi wanaohamaki.
“Ndiye aliyenifundisha habari ya kiongozi kutofanyia kazi tetesi vinginevyo unaweza ukawa unatengua uamuzi kila siku.”
Kwa mujibu wa Kibamba pia ni kiongozi anayeleta ari ya kufanya kazi miongoni mwa walio chini yake. Ana upendo, mpenda amani na mwanadiplomasia.
Kibamba anarejelea matamko ya TGNP aliyoshiriki kuandaa ikiwa ni sehemu ya kazi yake chini ya Rusimbi kwamba hayakuwa ya ‘kutunishiana misuli’.
Anasema yalikuwa ya mawasiliano ya kidiplomasia kiasi kwamba hata akikosoa, inaonekana mantiki ya kufanya hivyo.
Anamtaja kwamba ni muumini wa maridhiano kama ilivyo kwa Rais Samia Suluhu Hassan. “Hawa ni wanawake viongozi wanaopenda suluhu.”
Kiutendaji, Kibamba anasema Rusimbi ni mwasisi wa dhana ya bajeti yenye mlengo wa kijinsia uongozi wake tangu akiwa TGNP. Ni miongoni mwa maeneo aliyofanyia uchechemuzi wa kutosha.
“Ilikuwa ni faraja katika maisha yangu kufanya kazi na Mary Rusimbi… Anaacha alama kwangu na ana alama kubwa katika harakati za usawa wa klijinsia Tanzania,” anasema Kibamba.
‘Amenifunda nikafundika’
Nashivai Mollel ni Mkurugenzi wa taasisi ya Transforming Life inayojishughulisha na ulinzi na usalama wa mtoto. Yeye anamtaja Rusimbi kuwa ni mlezi wake.
Anasema amekuwa katika NGO kwa miaka 17 na Rusimbi amemuunga mkono kwa kiwango kikubwa.
Isome pia:‘Mpishi’ wa viongozi wanawake
Nashivai anasema Rusimbi amemuunganisha na majukwaa kadhaa ya wanawake. Mfano, Wanawake, Katiba na Uongozi pamoja na mtandao wa wanawake wa kupambana na rushwa ya ngono.
“Nimefahamu wadau wengi,” anasema Nashivai akishuhudia pia manufaa aliyopata WFT baada ya kuunganishwa na Rusimbi akimwelezea zaidi kuwa ni mama anayependa kusikiliza na kujibu kwa utulivu. Ni mahiri wa kusimamia ajenda yake.
Kwamba, Rusimbi ni muumini wa kuandaa watu walio nyuma yake kwa ajili ya kushika usukani baadaye.
Kwa ujumla, anamtaja mama huyu kuwa mshiriki mkubwa wa demokrasia na maendeleo ya usawa wa kinjinsia kutokana na ushiriki wake katika taasisi mbalimbali.
Kwa mujibu wa Nashivai, miongoni mwa mambo aliyojifunza kwa Rusimbi ni uongozi thabiti, kufanya kazi kwa bidii na kutenga muda wa kupumzika.
Nashivai anarejelea Kituo cha Nendiwe akisema kinadhihirisha dhana hiyo ya ‘kazi na mapumziko’ kwa vitendo kwani kinatoa faraja na amani ya moyo kwa mwanamke baada ya masaibu mbalimbali.
Ushuhuda wa Nashivai kwa Rusimbi unathibitisha kauli ya Rusimbi mwenye umri wa miaka 71 kwamba anapendelea ushirikiano katika kufanya mambo yenye manufaa.
Mfemenia mbobevu na Mkurugenzi Mkuu wa Hope Afrika kutoka nchini Zimbabwe, Hope Chigundu alikuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa kituo cha Ndendeiwe.
Yeye alisifu kituo hicho akisema ni muhimu kwa ustawi wa wanawake.
Rusimbi ni tunu
Mwanahabari mwandamizi nchini, Dereck Murusuri anamwelezea Rusimbi kuwa ni mama shujaa, mshauri, mwalimu, mchehemuzi, mwezeshaji ‘anayewapika’ wanawake na kuwaivisha kiuongozi.
“Nimekaa naye kwenye vikao vingi. Ni mbunifu, mbobevu wa masuala ya jinsia na maendeleo. Hata balozi mbalimbali alizofanya kazi, alikuwa akifanya kama mbobevu wa masuala ya jinsia,” anasema Murusuri.
Murusuri anasema kituo cha Nendiwe ni uthibitisho kwamba Rusimbi ni tunu ya mwanamke kwa maendeleo ya taifa..
Mwanamke mashuhuri
Mwandishi wa habari mwandamizi, Ezekiel Kamwaga katika makala yake ya uchambuzi iliyochapishwa BBC News Swahili Agosti 16, 2020 anamtaja Rusimbi kuwa miongoni mwa wanawake mashuhuri.
Katika makala hiyo: ‘Uchaguzi Tanzania 2020: Wanawake Kuweka Rekodi Mpya Mwaka Huu?’ Kamwaga anamjumuisha Rusimbi na wanawake waliopata umaarufu kutokana na harakati zao kupitia asasi za kiraia.
Anasema wengine mashuhuri wa miaka ya 1990 akisema walipata umaarufu na heshima si kwa kutumia vyama vya siasa, bali zaidi kupitia harakati zao kupitia asasi za kiraia.
Mkurugenzi wa taasisi ya Wanawake katika Jitihada za Kimaendeleo (Wajiki) ya Kinondani katika Mkoa wa Dar es salaam, Janeth Mawinza anasema: “Sina jina naloweza kumwita maana kwangu na kwa wanawake wengine, tumuite ‘Mama Mfuta Machozi na mrudisha ndoto zilizopotea. Amekuwa kiungo na daraja kubwa.”
Mawinza anasema Rusimbi amemjenga kiuongozi akimpatia elimu tangu alipokutana naye katika mkutano wa Mtandao wa Mashirika Yanayopinga Rushwa ya Ngono. Alimuidhinishia ufadhili wa kampeni ya ‘Vunja Ukimya, Safari Salama Bila Rushwa ya Ngono Inawezekana’.
Atuzwa kwa mafanikio
Septemba 5, 2017, TGNP Mtandao ilitoa tuzo kwa wanawake wapatao 20 vinara wa mafanikio katika ngazi mbalimbali mmoja wao akiwa Rusimbi.
Rais Samia Suluhu (wakati huo akiwa Makamu wa Rais), pia alikuwa miongoni mwa wanawake waliotunukiwa katika Tamasha la Jinsia la TGNP, Dar es Salaam.