Sababu za magonjwa ya misuli, mgongo hizi hapa

WAKALA wa Usalama na Afya Mahali pa kazi (OSHA), wametaja sababu za kuongezeka kwa magonjwa kazi ikiwemo misuli, mgongo , viuno na shingo kuwa yametokana na kutozingatiwa kwa usalama na afya maeneo mbalimbali ya kazi.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa OSHA, Hadija Mwenda amesema hayo Dar es Salaam leo wakati wa semina ya wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari (JOWUTA) iliyohusisha zaidi ya washiriki 50 kutoka Dar es Salaam na Pwani.

“Mtindo wa ukaaji, viti vinavyotumika kwenye maofisi vinapaswa kuzingatia usalama na afya. Lakini pia, ofisi husika zizingatie kanuni za Usalama na Afya vinginevyo kuna athari kubwa kiafya na kiuchumi baadaye kwa mfano kutumia fedha nyingi kujitibu na kuishia kuwa maskini,” amesema.

SOMA: ATE wasifu tozo nafuu Osha

Mwenda amesema hakuna mazingira ya kazi yasiyo na vihatarishi hivyo ni lazima Wakala hao kufanya ukaguzi wa mara kwa mara dhidi ya afya na usalama ili kuwalinda wafanyakazi dhidi ya magonjwa hayo.

Amesema tathmini waliyoifanya imebaini kuwa bado watanzania wana uelewa mdogo kuhusu sheria zao, hivyo kwa kutumia waandishi wa habari wanaamini watafikia watu wengi.

Wakili wa OSHA, Rehema Msekwa amesema kila mwajiri katika taasisi, kampuni na viwanda anapaswa kujisajili kwani kwa kukaa kimya wanafanya makosa ambayo yanaweza kuwagharimu.

Amesema kwa waajiri ambao hawana sera za Usalama na Afya Mahali pa kazi wakibainika wanaweza kutozwa faini ya sh 500,000 ya papo kwa papo.

Msekwa amesema wafanyakazi wana haki ya kufanyiwa vipimo na madaktari ambao wamepewa jukumu hilo na OSHA ili kubaini changamoto zao na kuwapangia maeneo sahihi ya kufanyia kazi.

Mwenyekiti wa JOWUTA, Mussa Juma amesema waandishi wa habari wanatakiwa kuwekewa mazingira bora kwa kufuata sheria ya usalama na afya mahali pa kazi.

Amesema kwa ujumla ofisi zote za waandishi wa habari hazina sera ya usalama na afya mahali pa kazi, hivyo waajiri wanapaswa kuzingatia ili wafanyakazi wao waweze kuwa salama.

Habari Zifananazo

Back to top button