Sakata la mgomo Kariakoo laibukia bungeni

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson.

SAKATA la mgomo wa wafanyabiashara ulioanza leo asubuhi katika soko la Kariakoo umeliteka Bunge, jijini Dodoma huku wabunge wakitaka serikali kueleza hatua zinazochukuliwa kuumaliza.

Akitumia Kanuni ya 54(1), Mbunge wa Makete Festo Sanga alilifahamisha Bunge juu ya suala la dharura linaloendelea Kariakoo, Dar es Salaam kuhusu mgomo wa wafanyabiashara katika soko hilo.

“Hivi ninavyozungumza, hakuna kinachoendelea katika soko lile (Kariakoo)….Kariakoo imebeba majimbo mengi…Mimi kama mbunge wa Makete, asilimia zaidi ya 50 ya wanafanyabiashara wanatoka Makete.

Advertisement

“Hivi ninavyozungumza kuna mgomo unaotokana na changamoto mbalimbali zikiwemo kamatakamata, Sheria ya Kodi (EFD) lakini kingine ni usajili wa stoo (maghala),” alieleza Sanga.

Katika hoja yake hiyo, Sanga alilifananisha soko hilo kubwa Afrika Mashariki na ‘Dubai ya Tanzania’ huku akisisitiza ikiwa shughuli zitasimama, nchi itakosa mapato.

Baada ya maelezo hayo, Spika Tulia Ackson alimtaka Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda, Dk Ashatu Kijaji kutoa maelezo.

Dk Kijaji alitumia muda kulieleza Bunge kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla na timu ya wataalam kutoka Wizara za Fedha na ile ya Viwanda na Biashara kuwa wapo kwenye majadiliano na uongozi wa wafanyabishara hao.

“Lakini kuna sehemu wafanyabiashara wanaendelea na shughuli zao kwa kutumia uhuru wao lakini kuna wengine wamefunga maduka,” Waziri alisema. 

Baada ya maelezo hayo, Dk Tulia aliomba apewe muda ili ajiridhishe juu ya sakata hilo huku akikiri kuwa uwepo wa kikao kati ya pande zote tajwa ni dhahiri kuwa kuna changamoto.

Alisisitiza: “Kwa kuwa Bunge linaendelea, tutapata muda wa kulitazama hili.”