Samia ahimiza kujiandikisha daftari la kura

RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka wanachama wa Chama cha Waandishi Waendesha Ofi si Tanzania (TAPSEA) wajiandikishe na kuhuisha taarifa zao kwenye daftari la kudumu la mpigakura.

Amesema hayo kupitia simu ya mkononi aliyompigia Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alipomwakilisha kwenye ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 12 wa Tapsea unaofanyika Arusha.

“Huu ni mwaka wetu maalumu wa kumrudisha mama ili tuendelee kufanya mambo yetu, nawaomba ambao hawajarekebisha taarifa zao na ambao hawajajiandikisha wafanye hivyo,” alisema Rais Samia jana na kuibua shangwe ya wajumbe waliohudhuria mkutano huo.

Aliupongeza uongozi wa Tapsea kwa kukuza chama hicho na kuahidi kufanyia kazi changamoto zinazowakabili.

“Nimemsikia mwenyekiti Zuhura (Maganga – Mwenyekiti wa Tapsea) anaomba uchumi ukikua tuongeze mshahara… fanyeni kazi muongeze uchumi na mnajua mama hana shida, uchumi ukikua basi warudishieni walioukuza uchumi,” alisema Rais Samia.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewataka wananchi wa mikoa 16 ya Tanzania Bara na Zanzibar wajitokeze kuboresha taarifa na kutazama daftari la awali lililobandikwa katika vituo walivyojiandikisha.

Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele alisema baada ya uboreshaji wa awamu ya pili, tume haitaboresha tena mpaka utakapofanyika uchaguzi Oktoba mwaka huu.

“Niwasisitize Watanzania wote katika mikoa hii 16, wajitokeze kuja kuboresha taarifa zao au kuja kujiandikisha… daftari litaboreshwa kuanzia Mei 16 (leo) mpaka Mei 22,” alisema.

Jaji Mwambegele alisema mzunguko wa pili wa uboreshaji utahusisha mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Pwani, Singida, Dodoma, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Mjini Magharibi, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Kaskazini Pemba na Kusini Pemba.

Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpigakura mara ya kwanza ulihusisha mikoa 15, mara ya pili mikoa 16 na mara ya tatu itahusisha vituo vya magereza na vyuo vya mafunzo.

Mikoa iliyohusika kwenye mzunguko wa kwanza wa uboreshaji ni Iringa, Geita, Kagera, Mara, Shinyanga, Mwanza, Simiyu, Rukwa, Tabora, Katavi, Kigoma, Ruvuma, Mbeya, Njombe na Songwe kuanzia Mei Mosi mpaka Mei 7, mwaka huu.

Mzunguko wa tatu wa uboreshaji wa daftari utahusisha vituo 130 kwenye magereza ya Tanzania Bara na vituo 10 vilivyopo katika vyuo vya mafunzo Zanzibar kwa wakati mmoja na utafanyika kwa siku saba kuanzia Juni 28 hadi Julai 4, 2025.

Habari Zifananazo

One Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button