Samia ahubiri amani, ‘afunika’ Mwanza

RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wa dini na wadau wa amani kuziponya nyoyo za Watanzania hasa wanapofarakana kuelekea kwenye uchaguzi mkuu ili nchi ibaki salama.

Rais Samia aliyasema hayo Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza alipofanya mkutano wa hadhara na Sungusungu, maofisa usafirishaji na wadau wa amani wa Kanda ya Ziwa.

“Wadau wa amani, viongozi wa dini, kikatiba Tanzania haina dini ila watu wa Tanzania wana dini zao, nashukuru kuunda umoja huu wa wadau wa amani unaoweza kushughulikia changamoto za kidini au migogoro inapojitokeza na kuacha nchi yetu salama,” alisema.

Aliongeza: “Nyie ndio madaktari wa nyoyo zetu naomba muendelee na kazi ya kulea na kuponya nyoyo zetu hasa pale tunapofarakana kipindi hiki tunapokwenda kwenye chaguzi, tutafarakana naomba muingie kuponya nyoyo zetu ili tuwe salama”.

Aliwataka Sungusungu kudumisha amani na kulinda maendeleo yaliyopatikana nchini huku akiwasisitiza kubeba sera za serikali na za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuzieleza vema kwa wananchi.

“Mfano juzi tumezindua chanjo ya mifugo Simiyu mueleze kwa wafugaji waitumie vizuri. Utunzaji wa amani, utulivu na usalama ndani ya nchi yetu ni jukumu letu sote, hivyo wana Sungusungu kwa vile nyie ni walinzi wa jadi wa mila zetu ambazo sio potofu nyie ndio walinzi wa mambo yote, tushirikiane ipasavyo katika utunzaji wa amani hasa katika kipindi hiki sote tuwe macho tuwe walinzi wa jamii na kote tunapoishi,” alisema.

Aliwapongeza Sungusungu kwa kufikisha miaka 42 nchini na zaidi kwa kuibuka upya na kujiimarisha na kufanya kazi karibu zaidi na jeshi la polisi. “Nami niseme niko nanyi na hasa kwa kuwa mmenipa utemi, asanteni,” alisema.

Rais Samia alisema maendeleo yaliyofanyika nchini ikiwemo kujenge barabara, reli ya kisasa, madaraja makubwa, umeme, maji, shule, hospitali yote yanahitaji kulindwa na kutunzwa ili kunufaisha Watanzania.

“Jambo lingine nawahamasisha Sungusungu kutoa ushirikiano kufanya kazi karibu zaidi na viongozi wenu wa mikoa, wakuu wa mikoa, wilaya na viongozi wa halmashauri katika sekta mbalimbali kama afya, elimu na mifugo,” alisema.

Aliongeza kuwa serikali imeboresha mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu hivyo alishauri waunde vikundi ili kunufaika na mikopo hiyo.

Kuhusu maofisa usafirishaji, Rais Samia aliwaahidi serikali itaendelea kuwawekea mazingira rahisi ya kutoa huduma zao na kuwataka kuwa makini na kulinda abiria wao huku wakijilinda wenyewe kwani kuna wanaofanya uhalifu kwa kisingizio cha ofisa usafirishaji.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button