Samia akerwa utegemezi wahisani utekelezaji miradi

RAIS Samia Suluhu Hassan ameeleza kukerwa na utaratibu wa kugharimia miradi kwa kuomba misaada nje ilihali inaweza kugharimiwa na fedha za ndani.
Sambamba na hilo, amesema masharti yanayotolewa na wahisani hayana msingi hivyo ni wakati wa taifa kutegemea zaidi makusanyo ya ndani zaidi kuliko misaada kutoka nje kugharimia miradi mbalimbali.
Rais Samia amesema hayo wilayani Bariadi mkoani Simiyu wakati akifungua jengo la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Simiyu lililogharimu Sh bilioni 9.483.
Alisema ili kuondokana na hali hiyo, watumishi wa TRA wanapaswa kufanya kazi kwa bidii ili kutimiza malengo ya serikali iliyojiwekea katika ukusanyaji wa mapato.
Aliongeza kuwa ni dhamira ya serikali kutumia fedha za ndani katika kugharimia miradi mbalimbali isipokuwa miradi mikubwa kama Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR).
Rais Samia aliwakumbusha watumishi wa TRA kuwa ili kutimiza malengo ya ukusanyaji wa mapato, ni lazima wakusanye kodi kwa maelewano bila kutumia nguvu ili walipakodi wote waone ni wajibu wao kulipa kodi kwa hiyari.
Alisema wafanyabiashara wote hawapaswi kuwa adui wa TRA bali wanatakiwa kuwa rafiki ili mwenye uwezo alipe kwa hiyari na mwenye madeni aitwe wakae pamoja wazungumze namna ya kulipa, ikibidi ndio matumizi ya nguvu yatumike.
“Zamani ukisikia TRA, kila mtu alitamani kwenda huko. Ukikaa miezi mitatu, sita umenona suti nzuri unang’aa lakini sasa ni TRA ya kukusanya kwa ajili ya nchi yetu hilo nawapongeza sana,” alisema.
Aliwaeleza kuwa enzi za kuvaa suti na kupandisha mabega kwa watumishi wa TRA bila kutekeleza kwa ufanisi majukumu yao imepitwa na wakati na sasa kinachotazamwa ni juhudi na bidii katika ukusanyaji wa mapato kwa ajili ya nchi.
“Uwepo wa majengo haya umeboresha hali ya utendaji kazi, nimeona majengo ni mazuri mno, lakini ndani kuna vitendea kazi vya kisasa. Kuna mifumo madhubuti inayowapa urahisi wa kufanya kazi zenu,” alisema Rais Samia.
Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo, hakuna sababu sasa ya kutofikia malengo ya ukusanyaji wa kodi kwani ameidhinisha wafanyakazi wapya zaidi ya 1,000 kujiunga na timu ya TRA.
Alisema ndiyo maana katika bajeti ya mwaka ujao serikali imeongeza kiwango cha makusanyo.
Rais Samia alisisitiza kuwa kutokana na namna serikali ilivyoboresha maslahi ya wafanyakazi wa TRA, hana wasiwasi na uwezo wa mamlaka wa kufikia lengo hilo kwa sababu tangu aingie madarakani takwimu zinaonesha kuwa kila mwaka makusanyo yanapanda zaidi kuliko kushuka.
“Katika makusanyo, tuko kwenye asilimia 98 hadi 99 na baadhi ya mikoa ndio wako 97 lakini kuna mikoa imepita asilimia 100, kwa hiyo nina uhakika malengo tuliyoweka tutayafikia mwaka ujao wa fedha,” alisema.
Alisema wilayani Bariadi pekee, serikali itazindua miradi sita ambayo yote imejengwa na fedha za ndani zilizotokana na makusanyo ya ndani na kusisitiza kuwa hata miradi yote nchini miradi mingi inatekelezwa kwa fedha za ndani isipokuwa miradi mikubwa kama SGR.
Alisema ni muhimu kwa nchi kutegemea rasilimali zake za ndani kwa sababu kutegemea misaada dunia sasa hivi ina changamoto nyingi zikiwemo vita, hali inayowafanya wasifanye vizuri kiuchumi kama Tanzania.
“Wakati mwingine tunafanya kufuru, Tanzania hii Mungu katupa madini, bahari, maziwa, ardhi nzuri na kila kitu akini bado tunangojea mtu mweupe aje achimbe apeleke kwao kiduchu atupatie wakati alivichukua huku kwetu, hakuna haja ya kufanya hivyo,” aliongeza.