RAIS Samia Suluhu Hassan amempongeza Keir Starmer kwa kuchaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza kupitia Chama cha Labour.
Kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa X, Rais Samia alieleza kuwa anatoa pongeze hizo kwa niaba ya serikali na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Natarajia kuendelea kwa ushirikiano wa Tanzania na Uingereza katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto za kidunia na kukuza maendeleo ya uchumi kwa ajili ya wananchi wa nchi zetu mbili,” alieleza Rais Samia.
Starmer amekiongoza chama cha Labour kushinda Uchaguzi Mkuu wa Uingereza baada ya kufikisha viti 326 vinavyohitajika.
Isome pia:https://habarileo.co.tz/samia-ampongeza-waziri-mkuu-mpya-uingereza/
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Rishi Sunak amekubali kuwajibika kwa kushindwa kipitia Chama cha Conservative na akasema kilichotokea ni sawa na uamuzi wa kutisha kwa chama chake.
Katika uchaguzi huo Labour inakadiriwa kuunda serikali ijayo yenye wingi wa viti 166 na Conservative wamepoteza zaidi ya viti 170 na wanatabiriwa kubakia na wabunge 136.
Sir Starmer alianza maisha yake ya kitaaluma kama wakili katika miaka ya 1990 na aliteuliwa mkurugenzi wa mashtaka ya umma na mwendesha mashtaka mkuu wa uhalifu nchini Uingereza mwaka 2008.
Alichaguliwa kwa mara ya kwanza katika Bunge la Holborn na St Pancras Kaskazini mwa London mwaka 2015 na alichukua uongozi wa Labour baada ya uchaguzi mkuu wa chama hicho mwaka 2019.