Samia ataka dini, teknolojia kujenga amani, umoja

DAR ES SALAAM; RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wa dini kutumia nyumba za ibada kujenga jamii yenye maadili na hofu ya Mungu.
Aidha, amewasihi viongozi hao na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuliombea taifa na kudumisha amani, utulivu na mshikamano.
Rais Samia alieleza hayo jana alipozungumza katika ufunguzi wa hema la kufanyia ibada la Kanisa la Calvary Assemblies of God (Arise and Shine), Dar es Salaam linaloongozwa na Mtume Boniface Mwamposa.
“Ni imani yangu kuwa hema hili litatumika kujenga jamii yenye maadili na hofu ya Mungu.Ni kupitia hofu ya Mungu wanadamu wanakuwa wanadamu; kuna mtu alisema kuna mwanadamu na wanywa damu, usipokuwa na hofu ya Mungu wewe ni mnywa damu,” alisema.
Aliwataka pia Watanzania kuliombea taifa liendelee kudumu katika amani, utulivu na mshikamano na kuwa tathmini iliyofanyika hivi karibuni imeonesha kuwa Tanzania ndiyo nchi ya kwanza Afrika ya Mashariki kuwa na utulivu na amani, jambo ambalo linapaswa kudumishwa.
“Niwaonbe tunapoelekea kwenye jambo kubwa lile kwenye demokrasia ya nchi twende kwa utulivu na mshikamano wetu, najua katika jambo lile makundi ni mengi. Nilikuwa nasoma taarifa ya chama changu waliochukua fomu za ubunge ni zaidi ya 4,000 na udiwani ni zaidi ya 30,000, ni makundi mengi kweli lakini tukimaliza shughuli za mchujo wote tunakuwa kitu kimoja,” alifafanua.
Aliwahimiza viongozi wa dini kutumia nafasi zao kuwaunganisha Watanzania hususani kipindi hiki cha maandalizi ya uchaguzi ikiwemo michujo ya wagombea wa nafasi mbalimbali za kisiasa kuepuka uvunjifi wa amani.
Alisema kumekuwa na mabadiliko makubwa yanayotokana na maendeleo ya teknolojia na kwamba jinsi watu wanavyoitumia ndivyo itakavyowabadilisha kwa mema au mabaya na kuagiza Tehama itumike kwa tahadhari ili kuilinda jamii isiporomoke.
“Tuitumie teknolojia kama nyenzo ya kujiendeleza kufikia malengo ya kiuchumi. Pia, nyumba za ibada endeleeni kutumia teknolojia, naona siku hizi kuna TV za dini na redio. Tusambaze elimu ya dini, maadili katika jamii na neno la Mungu,” alifafanua.
Alizishukuru taasisi za kidini kwa kuwa zimekuwa zikiguswa na madhila yanayokumba jamii na kuyashughulikia na kueleza kwamba huo ndiyo utumishi wa Mungu wenye maana.
“Mnapofanya haya Mungu naye anashusha baraka zake mfanye zaidi. Hema hili litakuwa chemchemi ya uzima kwa ajili ya wengi watakaoitwa na Kristo ili waokolewe, sitarajii hema hili litakwenda kudanganya watu wakati wote ila litakwenda kukaribisha Wakristo wapate neno la Mungu ili waokolewe,” aliongeza.
Alimpongeza Mtume Mwamposa kwa kazi kubwa, waliyoifanya ya kujenga hema la kisasa na kwamba hakutegemea kuwa lingekuwa kubwa namna hiyo na kwamba amepata funzo kutoka kwake.
Awali, uongozi wa kanisa hilo uliiomba serikali iangalie uwezekano wa kulifanya eneo hilo liwe la ibada kwa muda wa kudumu ambapo Rais Samia aliahidi kulifanyia kazi.
“Kuhusu ombi la serikali kuunga mkono jitihada za asasi za kidini kuhakikisha taifa linaendelea kuwa na amani niwahakikishie kwamba huu ndiyo mwelekeo wa serikali yetu,” alisema.
Kwa upande wake, Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alimshukuru Mtume Mwamposa na kanisa hilo kwa ujumla kwa maombi maalumu waliyomfanyia Rais Samia na kueleza kuwa ni jambo kubwa kwa kiongozi kwani yanampa nguvu.
“Nawashukuru kwa maombi mliyofanya kwa Rais wenu ni jambo kubwa mmefanya kwa kazi kubwa anayofanya, ukipata wenzako wanaokuombea unapata nguvu. Muendelee kuliombea taifa amani na utulivu, wenye jicho baya kwa nchi wasifanikiwe,” alisema