RAIS Samia Suluhu Hassan amemtaka Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe, kusimamia kwa umakini masuala ya milipuko ya magonjwa ndani ya nchi.
Rais Samia alitoa agizo hilo jana Ikulu, Dodoma wakati wa kuwaapisha majaji wanne wa Mahakama ya Rufaa na watendaji wengine wanne waliokula kiapo cha utumishi wa umma, akiwemo Dk Magembe, aliyeteuliwa hivi karibuni. “Grace (Dk Magembe) umekuwa mganga mkuu wa serikali, ni jukumu kubwa kweli kweli na jukumu linalotaka umakini.
Naomba haya mambo ya milipuko, milipuko, inayotokea ndani ya nchi yetu uende ukaisimamie vyema wewe na timu yako,” alisema Rais Samia. Aliongeza kuwa anaamini, Dk Magembe ataifanya kazi hiyo kwa weledi na kuiepusha nchi na tahadhari zisizo za lazima.
“Naomba haya mambo uyaangalie kwa umakini na kuhakikisha yanadhibitiwa kikamilifu,” alisisitiza Rais Samia. Dk Magembe amechukua nafasi ya Profesa Tumaini Nagu ambaye uteuzi wake ulitenguliwa. Magembe alikuwa Naibu Ka[1]tibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Aidha, Rais Samia aliwataka viongozi wengine walioapishwa kufanya kazi kwa weledi na kuwa[1]jibika kwa maeneo waliyopewa. “Wengine pia, naombeni mkawe game changer (wabadilisha mchezo), niwaombe kazi nzuri imefanywa, hakuna kurudi nyuma,” alisema. Katika maelekezo kwa viongozi wa mahakama, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa mhimili huo kuendelea kutoa haki kwa haraka na ufanisi.
Alimponge[1]za Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma kwa juhudi zake katika utoaji wa haki na matumizi ya teknolojia (Tehama) kwenye mhimili huo. “Jaji Mkuu, nikupongeze kwa utoaji haki na matumizi ya Tehama kwenye mhimili huo. Natambua kuna changamoto ila tumeshaanza kuchukua hatua, nikuahidi tena kuwa tutaendelea kushirikiana,” alisema Rais Samia.
Rais Samia alimuagiza Ka[1]mishna wa Maadili wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Sivangilwa Mwangesi, kuchukua hatua kali dhidi ya viongozi wanaokiuka maadili. “Jaji Mwangesi, kuwa na meno siku moja uniambie rais huyu anyukuliwe, ndio watu watakaa sawa,” alisema.
Kwa upande wake, Jaji Mkuu Profesa Juma alimshukuru, Rais Samia kwa kuwaongezea nguvu majaji wa Mahakama ya Rufaa akisema hatua hiyo itapunguza mlundikano wa mashauri na msongamano magerezani.
“Tunakushukuru kwa kutuongezea nguvu. Sasa hii nguvu itatafsiriwa kama ongezeko la majopo kutoka 11 hadi 12, na tutapunguza mlundikano wa mashauri na kuondoa msongamano kwenye magereza,” alisema Profesa Juma.
Aliongeza kuwa matumizi ya teknolojia mahakamani yameongeza ufanisi na kuwezesha baadhi ya rufani kusikilizwa kwa njia ya video, jambo ambalo pia limepunguza gharama na kuboresha usalama wa wafungwa.
Majaji walioapishwa ni Jaji Latifa Mansoor, Jaji George Masaju, Jaji Dk Deo Nangela na Jaji Dk Ubena Agatho. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alimkaribisha, Rais Samia na kuwataka viongozi walioapish[1]wa kuzingatia viapo vyao katika kutekeleza majukumu yao. Waolikula kiapo cha maadili ni pamoja na Dk Magembe na Mshauri wa rais wa masuala ya afya na tiba, Profesa Mohamed Janabi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Ramadhan Lwamo na Msaidizi wa Katibu wa Baraza la Mawaziri, Merick Luvinga.