Samia awaita wawekezaji viwanda kuchakata pamba nchini

RAIS Samia Suluhu Hassan amewaomba wawekezaji wa viwanda vya kuchakata pamba wahakikishe wanatumia pamba inayolimwa nchini ili kuwapa wakulima soko la uhakika.

Alitoa rai hiyo jana wilayani Maswa mkoani Simiyu alipokuwa akizungumza na wananchi kupitia mkutano wa hadhara baada ya kufungua Kiwanda cha kuchakata pamba mbegu cha Shree Ragendra.

Alisema Mkoa wa Simiyu umejaliwa viwanda vingi vya pamba ambavyo vimekuwa chanzo kizuri cha ajira kwa wananchi wa mkoa huo na kwamba kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuchakata tani 350 za pamba mbegu kila siku.

“Kiwanda hiki kitaongeza thamani ya pamba na kuhakikisha soko la pamba tunayoilima ndani ya wilaya yetu kwamba pamba yote itakayolimwa kiwanda kile kina uwezo wa kununua, hivyo kuhakikisha soko la pamba kwenye wilaya yetu,” aliongeza.

Alieleza kuwa kiwanda hicho chenye thamani ya Sh bilioni 12 kitakuwa chanzo kizuri cha ajira kwa wananchi wa Maswa na pia chanzo cha uhakika cha soko la pamba yote inayolimwa katika wilaya hiyo.

Aidha, Rais Samia alisema kutokana na viwanda alivyozindua mkoani Simiyu, mkoa huo unatarajia kuchakata pamba mbegu tani 275,000 huku Wilaya ya Maswa ikitarajiwa kuvuna tani 65,000.

Miongoni mwa viwanda vilivyojengwa mkoani Simiyu ni pamoja na kiwanda cha chaki ambacho ndilo tegemeo la taifa kwa bidhaa hiyo.

Kutokana na ukweli huo, Rais Samia aliitaka Halmashauri ya Maswa kutenga eneo zaidi kwa ajili ya kiwanda hicho kuhifadhi malighafi nyingi zaidi ya chaki.

Kuhusu ulipaji kodi, Rais Samia aliipongeza Wilaya ya Maswa kwa kufanya vizuri katika makusanyo ya kodi na tozo ambapo imefanya vizuri kwa asilimia 96 na kuwataka wananchi waendelee kulipa kodi kwa maendeleo yao.

Katika eneo la miundombinu, Rais Samia aliwataka wananchi wa Maswa kutumia Reli ya Kisasa (SGR) ambayo imejenga kituo chake kikubwa katika eneo la Malampaka kuyafikia masoko zaidi kwa ajili ya mazao yao.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa alisema serikali imejenga shule zake karibu na makazi ya watu ili kuwa rahisi kwa wanafunzi kwenda shule.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button