Samia: Chagueni waadilifu, wabunifu

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi kutumia haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi waadilifu, wabunifu na wenye maono ya kuendeleza jamii.

Aidha, amesema uamuzi wa wapigakura utaheshimiwa kwa kuwa demokrasia yenye nguvu hujengwa kwa misingi ya heshima na mshikamano.

Alisema hayo Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma jana alipohutubia taifa kwa njia ya televisheni kuwaeleza wananchi umuhimu wa kupiga kura kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa leo.

Advertisement

Rais Samia alisema kila kura ina umuhimu katika kuamua mustakabali wa maendeleo ya taifa kwa kuwa itasaidia kufanikisha azma ya kujenga jamii yenye haki, usawa na maendeleo kwa wote.

Alisema haki hiyo ya kikatiba ni fursa muhimu kwa kila Mtanzania mwenye sifa ya kupiga kura kuchangia maendeleo ya nchi kwa njia ya kidemokrasia kwa kuchagua viongozi wenye sifa.

Rais Samia alisema serikali za mitaa ni msingi wa ujenzi wa taifa imara na lenye maendeleo endelevu.

Alisema kupitia viongozi wanaochaguliwa, nchi inajengewa misingi ya uwajibikaji, utoaji wa huduma bora kwa wananchi na usimamizi wa rasilimali za umma.

Isome pia:Viongozi vyama vya siasa wasisitiza amani

Alisema uchaguzi huo ni fursa ya kuhakikisha kuwa uamuzi unaohusu jamii unatokana na mahitaji yao halisi.

Aidha, Rais Samia aliwakumbusha wananchi watumie haki hiyo kwa utulivu ili kulinda amani na heshima ya taifa.

“Uchaguzi ni haki yetu na ni jukumu letu kuhakikisha tunatumia haki hiyo kwa utulivu, hivyo niwasihi wananchi tujiepushe na vitendo vya uchochezi, vurugu na uvunjifu wa sheria. Amani ni urithi wetu wa thamani na ni wajibu wetu kuulinda kwa gharama yoyote,” alisema.

Kuhusu kuheshimu uamuzi wa wapigakura, rais aliwataka viongozi wa vyama vya siasa, wagombea na mawakala wa uchaguzi wazingatie na kuheshimu sheria na kanuni za uchaguzi zilizowekwa ili kuwa na uchaguzi wa amani na utulivu.

Rais Samia aliwataka wasimamizi wa uchaguzi na wote wanaohusika kuhakikisha unafanyika kwa haki, uwazi na kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa na wadau.

“Ni matumaini yangu kwamba mtaendelea kutekeleza majukumu yenu kwa weledi, kulinda haki za wananchi na kudumisha utulivu tunapoelekea mwisho wa mchakato huu, ni dhamira ya serikali kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uwazi, haki na kwa kuzingatia kanuni za uchaguzi zilizopo,” alisema.

Alitoa rai kwa kila mdau anayeshiriki uchaguzi huo kutoa ushirikiano ili kufanikisha azma ya kuwa na uchaguzi wa amani unaoakisi heshima ya Tanzania, kama taifa lenye mshikamano na demokrasia imara.