Samia: Diaspora wametuma tril 2.5/- nyumbani

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema Watanzania wanaoishi nje ya nchi (diaspora) wamekuwa na mchango mkubwa kwa nchi kupitia fedha wanazotuma na uwekezaji.

Kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa twitter, Rais Samia amesema baada ya Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Troika jijini Windhoek nchini Namibia, alizungumza na Watanzania wanaoishi nchini humo baadhi wakiwa na familia zao.

“Ndugu zetu hawa kama walivyo Watanzania wengine waishio kwenye maeneo mbalimbali duniani, wamekuwa na mchango mkubwa kwa nchi yetu kupitia fedha wanazotuma nchini kusaidia ndugu na jamaa (zaidi ya shilingi trilioni 2.5 kwa mwaka jana) na uwekezaji katika maeneo mbalimbali,” ameandika Rais Samia.

Miezi kadhaa iliyopita, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango wakati anazungumza na Watanzania wanaoishi nchini Singapore, alisema serikali inatambua mchango wa diaspora katika ujenzi wa taifa.

Dk Mpango alisema kuanzishwa na idara maalumu inayoshughulikia masuala ya Watanzania wanaoishi nje ya Tanzania katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ni ishara ya kutambua mchango wa diaspora.

Miezi kadhaa iliyopita wakati akihutubia katika mkutano wa Rais Samia na mabalozi uliofanyika Zanzibar, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax alisema mchango wa diaspora umeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka.

Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), fedha zilizotumwa na diaspora zimeongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 400 mwaka 2020 hadi dola milioni 569.3 mwaka 2022.

Dk Tax pia alisema diaspora wamewekeza Sh bilioni 3.9 katika Dhamana ya Uwekezaji Tanzania (UTT) na wamenunua nyumba zenye thamani ya Sh bilioni 2.3 nchini.

Kwa mujibu wa Dk Tax, wizara inaendelea na maandalizi ya mfumo wa kidijiti ili kutunza taarifa za diaspora na taasisi za fedha kama benki nao wanashirikiana katika matumizi ya mfumo huo wa kidijiti.

Machi 23, mwaka huu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilisema imepata mkandarasi wa kutengeneza mfumo wa kuwasajili na kuingiza taarifa za diaspora wote waishio nje ya nchi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button