Samia, wenzake walaani machafuko DR Congo

RAIS Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), wamekutana mjini Harare, Zimbabwe kujadili hali ya amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Kwa muda mrefu serikali ya DRC imekuwa kwenye vita na jeshi la M23 likidhibiti jimbo la Goma na kwa sasa linaelekea Kusini kuchukua maeneo zaidi.

Advertisement

Rais Samia ndiye Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (TROICA) ambayo majukumu yake ni kutoa msingi wa amani na utulivu katika ukanda huo kama sharti la kufikia malengo la Jumuiya hiyo ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi, kutokomeza umasikini na ushirikiano wa kikanda kama ilivyoelezwa katika dira ya SADC 2050 na Mpango Elekezi wa Maendeleo ya Kikanda (RISDP) 2020-2030.

SOMA: Rais Samia awasili Zimbabwe kuhudhuria mkutano SADC

Pia, asasi hiyo inaongozwa na itifaki ya ushirikiano wa siasa, ulinzi na usalama ambayo inalenga kukuza amani na usalama katika SADC, kulinda watu wa kanda kutokana na kukosekana kwa utulivu kutokana na kuvunjika kwa sheria na utulivu, kuandaa sera ya pamoja ya nje ya kanda na kushirikiana katika masuala ya usalama na ulinzi.

Akizungumza wakati akifungua kikao hicho cha dharura, Mwenyekiti wa SADC na Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa alisema jumuiya hiyo haifurahishwi na hali ya kukosekana kwa amani inayoendeela DRC.

“Kwa niaba ya SADC na watu wa Zimbabwe natoa pole kwa wananchi wote wa DRC waliopoteza wapendwa wao na pia, askari waliopoteza maisha yao kwenye vita hiyo,” alisema.

“Jumuiya hii (SADC) itafanya kila inaloweza kusapoti harakati za kuiokoa DRC kwenye vita hii… lazima tufanye kitu zaidi kuinusuru DRC watu wake wametaabika sana na wanataabika, lazima amani ipatikane… nina imani mkutano wetu utakuja na suluhisho,” alisema.

Mnangagwa aliwashukuru na kuwapongeza wajumbe wa jumuiya hiyo kujitokeza kwenye kikao hicho cha dharura licha ya kupata ujumbe ndani ya muda mfupi.

Katika harakati za kumaliza vita DRC, juzi Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), William Ruto aliita kikao cha dharura na wanachama wa Jumuiya hiyo kilichofanyika kwa njia ya mtandao.

Katika kikao hicho viongozi hao wa EAC waliiagiza DRC kushirikiana na wadau, likiwemo kundi la M23 na majeshi mengine kufanya mazungumzo ya kuleta amani na kumaliza mgogoro unaoendelea.

Hata hivyo, katika kikao hicho Rais wa Congo, Felix Tshisekedi hakushiriki na kutoa udhuru.

Tshisekedi amekuwa akikataa kuzungumza moja kwa moja na M23 akisisitiza kuzungumza na Rwanda pekee.

Viongozi hao wa EAC pia, walitoa wito wa kufanyika kwa mkutano wa pamoja wa Jumuiya hiyo na SADC kuona njia nyingine ya kusaidia kumaliza mzozo huo.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *