Sangara wapungua Ziwa Victoria

SAMAKI aina ya sangara wamepungua katika Ziwa Victoria kutoka tani 537,479 mwaka 2020 hadi tani 335,170 kwa mwaka 2021.

Ofisa Uvuvi wa Mkoa wa Mwanza, Titus Kilo alisema hayo alipokuwa akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya sekta ya uvuvi na mikakati ya kuboresha sekta hiyo kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Mwanza.

Alisema kupungua kwa samaki hao kumegundulika kutokana na tathimini ya kubaini wingi wa samaki ziwani iliyofanyika kati ya mwaka 2020 na 2021.

Alisema kushuka kwa idadi ya sangara katika Ziwa Victoria kumetokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa shughuli za uvuvi na uvuvi haramu.

Alisema sangara wengi walioko ziwani kwa sasa ni sangara wadogo wenye urefu wa chini ya sentimeta 50. Hata hivyo alisema dagaa wameongezeka kutoka tani 430,359 mwaka 2020 hadi tani 557,479 mwaka 2021.

Alisema pia samaki aina ya furu nao wameongezeka kutoka tani 281,283 mwaka 2020 hadi kufikia tani 360,380 mwaka 2021. Alisema kuongezeka kwa dagaa na furu kumetokana na kupungua kwa sangara ziwani ambao huwala dagaa na samaki wadogo kama furu kwa wingi.

Kwa upande wa udhibiti wa uvuvi haramu katika ziwa hilo kubwa Afrika, alisema halmashauri saba zinazozunguka Ziwa Victoria zilifanya jumla ya doria 186 katika kipindi Julai 2021 hadi Juni mwaka huu na kuweza kukamatwa zana haramu za uvuvi 3,507.

Alizitaja zana zilizokamatwa kuwa ni pamoja na nyavu za kokoro 188, nyavu za timba 1,270, nyavu za makila 734, nyavu za dagaa 47, kimea 96, katuli 96 na ndoano 700.

Aliongeza kuwa mitumbwi 102, watuhumiwa 11 wa samaki wachanga wasiofaa kuvuliwa aina ya sato kilo 228 na sangara kilo 8,752 vilikamatwa katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Mwanza.

Aidha alisema katika kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka huu doria 78 zilifanyika na kuwezesha kukamatwa kwa zana haramu 937 zikiwemo nyavu za kokoro za sangara 206, nyavu saba za kuvua dagaa, nyavu 411 za timba, nyavu za makila 128 ambazo ni nyavu za kurusha, kimea au migono 39 na katuli au kaduli ambao ni uvuvi wa kutumia baruti 21.

Alisema mitumbwi 100, watuhumiwa 12 na samaki wachanga wasiofaa kuvuliwa aina ya sato kilo nne na sangara kilo 2,062 walikamatwa kutoka kwa watu wanaojihusisha na uvuvi haramu.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button