RAIS Samia Suluhu Hassan amesema maboresho ya Sera ya Ardhi ya Mwaka 1995, yatawezesha kufanyika mambo sita ikiwa ni pamoja na kutambua fursa kwenye uchumi wa buluu.
Pia, amesema sera mpya ya ardhi itajumuisha na kuyapa misingi ya kisera masuala ambayo hayakuzingatiwa na sera iliyopita.
Amesema hayo Dodoma wakati wa uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Ardhi ya Mwaka 1995, Toleo la Mwaka 2023.
Rais Samia alisema wakati wa utekelezaji wa sera ya awali baadhi ya shughuli zilifanyika bila kuwa na msingi wa sera ikiwemo kazi ya kuimarisha mipaka ya kimataifa ya Tanzania na nchi jirani katika kurahisisha utambuzi wa alama za mipaka.
Alisema serikali imeamua kuliweka jambo hilo katika sera ili kuipa nguvu katika utendaji na pia nguvu ya kutunga au kurekebisha sheria ya mipaka ya Tanzania.
Rais Samia alisema kwa kutambua fursa kwenye uchumi wa buluu, sera imebainisha haja ya kuweka utaratibu wa kisera wa kusimamia uchumi wa rasilimali zilizoko kwenye maji kwa kupima na kumilikisha ardhi katika maji.
“Tunakwenda sasa kupima rasilimali zetu katika maji, kuna diplomasia ya kutosha lazima itumike ili kuelewana na majirani ili tuweze kupima na tujue Tanzania tunakwenda mpaka wapi na kuviepusha vizazi vijavyo na migogoro ya ardhi ya mipaka huko baadaye,”alisema.
Pia, Rais Samia alisema wawekezaji wanatamani kuja kuwekeza katika mradi wa sekta ya nyumba lakini wakakwamishwa na sera ya ardhi.
Alisema sera ya awali haikuruhusu uwekezaji katika milki ya ardhi kutoka nje ya nchi na kukwamisha jitihada za kuvutia mitaji kutoka nje kuwekezwa katika sekta ya milki ikiwemo ujenzi wa makazi ya bei nafuu unaozingatia nafasi kama kuanza ujenzi wa ghorofa vijijini.
Alihimiza wawekezaji hao waje kujenga makazi kwa sababu sera itaongozwa na sheria inayoruhusu wakodishwe ardhi ili watatue tatizo la makazi.
Aidha, Rais Samia alisema sera mpya ya ardhi itaongeza kasi ya upimaji na usajili wa ardhi.
Alisema licha ya hatua iliyopigwa katika sekta ya ardhi takwimu zinaonesha asilimia 75 ya ardhi nchini bado haijasajiliwa.
Rais Samia alisema hali hiyo si tu kuwa inachangia upotevu wa mapato bali pia inaleta hali ya kutokuwa na usawa kwa kuwa baadhi ya wamiliki wanalipia umiliki wa ardhi na wengine hawalipii.
“Hii si sawa na si haki, katika hili tumebaini kuwa sera iliyopita haikuwa na sharti la kuwataka wamiliki kusajili ardhi yao, sasa tunataka kila kipande cha ardhi ndani ya nchi hii kipangwe, kipimwe na kisajiliwe kwa kila mmoja ili mwaka ukizunguka ailipie ardhi hiyo,” alisema.
Rais Samia alisema serikali itahakikisha kazi ya upangaji, upimaji na usajili wa ardhi inarahisishwa ili kuwawezesha wananchi kumiliki ardhi.
Alisema pamoja na kusajili kila kipande cha ardhi, serikali itaongeza usalama wa umiliki wa ardhi ili kudhibiti migogoro ya ardhi nchini pamoja na matapeli wanaobadili hati za ardhi na kumfanya mwenye haki kunyang’anywa haki yake.
Rais Samia alisema serikali kupitia sera mpya ya ardhi itasaidia kutatua migogoro ya ardhi na akasema kuna mafanikio katika utatuzi wa migogoro ya ardhi kwa kuunda mabaraza ya ardhi ngazi ya kijiji, kata na wilaya.
Alisema sera hiyo itatumia teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) kudhibiti mifumo ya migogoro na itadhibiti wanaoenda kutafuta mafaili maktaba kwa kuwa mifumo inasomana hivyo matapeli watashindwa kurubuni watu.
Rais alisema pia itaimarisha uthamini na ulipaji wa fidia kwa sababu serikali imebaini upungufu katika utaratibu wa ulipaji wa fidia ya ardhi na mali na kusababisha malalamiko makubwa kuhusu upimaji, uthamini na mapunjo ya fidia.
Alitaja tija ya tano ni kuimarisha uwekezaji katika uendelezaji wa ardhi kutokana na uhitaji wa makazi bora ndani ya nchi hivyo uwekezaji zaidi unahitajika na itaimarisha utunzaji wa taarifa kwenye sekta ya ardhi kuongeza na kuimarisha utendaji kazi na kuziba mianya ya upotevu wa mapato.