DODOMA – SERA ya Elimu na Mafunzo 2014, Tolea la 2023 imekuja na malengo mahsusi saba. Kwa ujumla malengo hayo yanataka uwepo mfumo wa elimu na mafunzo unaowezesha kuwaandaa Watanzania wenye maarifa, stadi na mtazamo chanya kuchangia maendeleo endelevu ya taifa.
Rais Samia Suluhu Hassan alizundua sera hiyo na mitaala iliyoboreshwa Dodoma juzi na kuagiza wizara husika kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sera na mitaala ili kuleta matokeo yaliyokusidiwa.
Wizara zilizopewa maagizo hayo ni Wizara ya Fedha, Wizara ya Mipango na Uwekezaji, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Sera hiyo ina lengo la kuwa na mfumo, muundo na utaratibu nyumbufu wa kumwezesha kila Mtanzania kujiendeleza kwa njia mbalimbali kitaaluma na kitaalamu.
Pia, ina lengo la kutoa kutoa fursa mbalimbali za elimu na mafunzo nchini. Sera hiyo pia ina lengo la kuwa na elimu na mafunzo yenye viwango vya ubora unaotambulika kitaifa, kikanda na kimataifa.
Pia, ina lengo la kuwa na rasilimali ya kutosha na yenye umahiri na weledi stahiki kuendana na vipaumbele vya taifa.
Jambo la tano ni kuwa na usimamizi na uendeshaji madhubuti wa elimu na mafunzo nchini. Lengo la sita ni kuwa na mfumo endelevu wa ugharamiaji wa elimu na mafunzo na saba ni kuwa na mfumo wa elimu na mafunzo unaozingatia masuala mtambuka.
Matamko 11 Katika sera hiyo kuna matamko 11 likiwemo la serikali kuwa itaweka mfumo nyumbufu wa elimu na mafunzo ili kuwezesha wananchi wengi zaidi kujielimisha na kuwa huru kutafuta elimu katika fani wanazopenda.
Wananchi wataweza kutumia njia mbalimbali za kupata elimu na mafunzo ikiwemo huria na masafa kulingana na stahili na uwezo wao. Tamko la pili ni kuwa mfumo wa elimu utajikita katika kujenga umahiri.
Katika hilo msisitizo utakuwa kupata ujuzi, maarifa, weledi, mwelekeo, mitazamo chanya, maadili mema na tabia zinazokubalika kulingana na mahitaji ya taifa na ulimwengu wa kazi pamoja na kuzingatia mfumo wa tuzo wa taifa.
Tamko la tatu ni kuwa elimu katika mfumo rasmi itagawanyika katika ngaz