Serikali kugeuza mafuriko ya maji kuwa fursa kiangazi

SERIKALI imeanzisha programu ya kugeuza maji ya mafuriko kuwa fursa kwa wananchi ya kuimarisha ustawi wa wananchi kupitia kilimo cha umwagiliaji, uvuvi, maji safi pamoja na mifugo.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alisema hayo jana wilayani Busega mkoani Simiyu wakati wa ufunguzi wa Mradi wa Maji wa Lamadi wenye thamani ya Sh bilioni 12.83.
Alisema katika maeneo mengi mvua zimekuwa zikisababisha maafa kutokana na mafuriko makubwa yaliyogharimu maisha ya wananchi pamoja na mazao.
Aliongeza kuwa programu hiyo inaenda kukusanya maji hayo na kuyahifadhi kwa ajili ya matumizi ya baadaye wakati wa kiangazi hali itakayosaidia kutatua shida ya maji.
Aidha, alisema hatua ya Rais Samia kupeleka maji ya Ziwa Victoria mkoani Simiyu, ametekeleza kwa vitendo ajenda ya wabunge wa Kanda ya Ziwa ya kuyatumia maji ya ziwa hilo kukabiliana na changamoto mbalimbali.
“Ajenda ya wabunge wa Kanda ya Ziwa ilikuwa maji ya Ziwa Victoria yatumike katika kutatua matatizo ya wananchi, Rais (Samia) umetoa zaidi ya Shilingi bilioni 33 kwa ajili ya wananchi wa Bukoba mkoani Kagera wapate maji hayo,” alisema Aweso.
Alisema katika Mkoa wa Mara, serikali imetoa Sh bilioni 44 kwa ajili ya kupeleka maji ya Ziwa Victoria ili kukabiliana na changamoto mbalimbali za mkoa huo.
Aweso alisema Serikali ya Awamu ya Sita imefikisha maji kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kutoka Ziwa Victoria, ambao ni mradi wenye thamani ya Sh bilioni 70 na kuwasaidia wananchi wa mkoa huo kupata maji safi na salama.