Serikali kuimarisha mazingira ya uwekezaji

DAR ES SALAAM: SERIKALI imesema itaendelea kuboresha mazingira ya wawekezaji ili kuimarisha uchumi wa nchi na kupunguza wimbi la ukosefu wa ajira, hususan kwa vijana.
Kauli hiyo imetolewa Juni 19,2025 na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, wakati wa uzinduzi wa mgahawa mpya wa KFC uliopo katika kituo cha mafuta cha TotalEnergies kilichopo Shekilango, Ubungo, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla hiyo, Msando amesema ni jambo la kujivunia kuona uwekezaji mkubwa kama huo unafanyika ndani ya Wilaya ya Ubungo, kwani mbali na kutoa huduma bora kwa wananchi, pia utachangia kuongeza pato la halmashauri kupitia ulipaji wa kodi na tozo mbalimbali, hivyo kuleta maendeleo ya kiuchumi.
“Ni mevutiwa sana na jitihada zenu za kuwekeza katika wilaya yetu. Rais Samia Suluhu Hassan, amekuwa mstari wa mbele kuvutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi,na uwekezaji huu ni dhahiri kuwa utasaidia kupunguza changamoto ya ajira kwa vijana. Nimesikia tayari mmewaajiri vijana zaidi ya 800 hili ni jambo la kutia moyo,” amesema Msando.
Aidha, amewahimiza wawekezaji kuendelea kufanya tafiti katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es Salaam kwa lengo la kuwekeza kwa wigo mpana zaidi, huku akiwahakikishia ushirikiano kutoka kwa uongozi wa wilaya na mkoa katika kutatua changamoto zitakazojitokeza.
Katika hatua nyingine, Msando ametoa rai kwa wananchi na wadau mbalimbali kuendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam, akisisitiza kuwa ni marufuku kwa magari kutanua barabarani kwani ndiyo chanzo kikuu cha foleni na atakae bainika sheria kali zitachukuliwa dhidi yake.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Dough Works Limited (DWL), Vikram Desai amesema uwepo wa mgahawa huo mpya si kwa ajili ya kutoa chakula tu, bali pia ni sehemu ya ajenda yao ya kutoa ajira, kusaidia jamii, na kuleta huduma za kiwango cha kimataifa katika maisha ya kila siku ya Watanzania.
“Uzinduzi huu ni matokeo ya ushirikiano wa kimkakati kati ya DWL na TotalEnergies Tanzania. Ushirikiano huu unalenga kutoa huduma zinazogusa kila kipengele cha maisha ya mteja kutoka kujaza mafuta, kupata chakula cha haraka, hadi ununuzi wa bidhaa za rejareja mahali pamoja,” amesema Desai.
Aliongeza kuwa kampuni hiyo ina zaidi ya wafanyakazi 800 na imeanzisha matawi 30 katika miji ya Dar es Salaam, Dodoma, na Arusha, huku kila tawi jipya likichangia ajira, ukuzaji wa ujuzi, na maendeleo ya sekta ya huduma za chakula nchini.
Naye Mkurugenzi wa Mitandao kutoka TotalEnergies Tanzania, Abdulrahim Siddique, akimuwakilisha Mkurungenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo,Mamadou Ngom amesema uzinduzi huo wa mgahawa mpya wa KFC ni sehemu ya mkakati wa kampuni yao wa kuboresha uzoefu wa mteja kwa kuchanganya ubora, ufanisi, na faraja katika kila huduma inayotolewa.
“Kwa kuongeza mgahawa huu katika kituo chetu cha Ubungo, tunaleta si tu chapa inayopendwa duniani, bali pia tunaendeleza ahadi ya kutoa huduma za kiwango cha juu kwa wateja wetu. Hii ni ishara ya dhamira yetu ya pamoja na Dough Works ya kuwapa wateja huduma zaidi ya mafuta,” amesema Siddique.
Amesema lengo la TotalEnergies ni kuendelea kuleta huduma bora na za thamani kwa wateja wake kote nchini Tanzania, kupitia ubunifu na ushirikiano wa kimkakati na wadau wa huduma mbalimbali.