Serikali kuingiza bil 2.5/-uwindaji wa kitalii

DAR ES SALAAM: SERIKALI ya Tanzania inatarajia kuingiza Dola 968,000 sawa na Sh bilioni 2.5 na mapato mengine kama ada ya vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa mwaka.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk Pindi Chana ametoa taarifa hiyo leo Februari 21,2025 katika hafla ya kukabidhi vyeti vya umiliki wa vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa wawekezaji wanne iliyofanyika Dar es Salaam.

“Ninayo furaha kukabidhi vyeti hivi kwa wawekezaji ambao ni K&F Wild Expedition Ltd kwa Kilwa Open Area Nakiu, Michel Mantheakis Safaris Ltd kwa Muhesi GR, Out of Africa Ltd kwa Lwafi Nkamba, Royal Conservation Ltd kwa Pori la Akiba la Pololeti na Selous MT2 kwa Neon Investment Ltd chini ya Uwekezaji mahiri kwenye Maeneo ya Wanyamapori (Special Wildlife Investment Concession Areas-SWICA),” amesema Chana.

Dk Chana amesema utoaji wa vyeti hivyo kwa wawekezaji unaendana na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokana na kwamba inahalalisha umuhimu wa tasnia ya uwindaji kwa uchumi wa nchi.

Aidha, amewakaribisha wawekezaji wengine kutoka China na mataifa mengine kuwekeza katika utalii huku akimpongeza Samia Suluhu Hassan kwa mpango wa kuitangaza Tanzania katika kiwango cha kimataifa kupitia filamu za “Amazing Tanzania” na “Tanzania, The Royal Tour”.

SOMA ZAIDI: Tanzania, Marekani zajadili uwindaji njia ya mtandao

“Napenda kuwahakikishia wadau wote wa uwindaji kwamba dhamira ya serikali ni kuendelea kuweka na kudumisha mazingira wezeshi ya biashara zao bila kuathiri uhifadhi na ustawi wa watu wetu,” amesema Chana.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Tawa, Meja Jenerali Mstaafu Hamis Rajabu Semfuko amesema kuwa Tawa imekuwa ikitumia mikakati ya kimasoko kuvutia wawekezaji kutoka duniani kote ikiwa ni pamoja na matumizi ya mnada wa kielektroniki wa vitalu vya uwindaji ambapo kwa mara ya kwanza imefanikiwa kupata wawekezaji kutoka China katika sekta ya uwindaji.

“Tawa imejipanga vyema ili kufikia soko la kimataifa na soko la ndani la utalii sambamba na kuangalia uwezekano wa masoko ya mapya ya utalii kama China, Urusi na Brazili,” amesema Meja Semfuko.

Kwa upande wake, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Mlage Kabange alifafanua kuwa katika jitihada za kuvutia wawekezaji na watalii zaidi, TAWA itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button