Serikali kujenga mtandao mkubwa mabomba ya gesi

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema lengo la serikali ni kuwa na mtandao mkubwa wa mabomba ya gesi pamoja na vituo vya kujazia gesi kwenye magari ili kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa urahisi.

Dk Biteko ameeleza hayo leo Machi 6, 2025 alipofanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Rashal Energies, Farhiya Warsame kando ya Kongamano na Maonesho ya Petroli ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAPCE’25) linalofanyika kwa  siku tatu jijini Dar es Salaam.

Kampuni ya Rashal Energies, ndio inayojenga bomba la gesi kutoka Kisemvule hadi Mbagala jijini Dar es Salaam kwa ajili ya matumizi ya vituo vya kujazia gesi kwenye magari (CNG) na kwenye viwanda.

Dk Biteko ameeleza kuwa serikali ipo tayari wakati wowote kutoa ushirikiano kwa kampuni zinazotaka kuwekeza kwenye kutoa huduma hiyo kwa wananchi.

Kwa upande wake, Farhiya Warsame amemshukuru Dk Biteko kwa miongozo yake ambayo imepelekea kampuni hiyo kuanza kutekeleza mradi huo.

Ameeleza kuwa wananchi wameonesha mwamko mkubwa kwenye kuendesha vyombo vyao vya usafiri kwa kutumia gesi asilia badala ya mafuta kutokana na gesi asilia kuwa na gharama nafuu kuliko mafuta.

Vilevile, Dk Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa kampuni ya Rock Mountain ya nchini Canada, Nick Lenstra ambayo imesaini Mkataba wa Ushirikiano na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa ajili ya kuanza kazi za upembuzi yakinifu na kuzungumza na wadau wa ndani ikiwemo Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) ili kutumia gesi asilia kutengeneza nishati kwa njia ya kimiminika ambayo inaweza kutumika kwenye ndege.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button