DAR ES SALAAM: SERIKALI imepanga kuongeza kiwango cha pato la taifa kufikia asilimia 15 ifikapo mwaka 2026/2027, katika jitihada za kuboresha uwezo wa kugharamia miradi ya maendeleo na kupunguza utegemezi wa mikopo na misaada.
Akizungumza na waandishi wa habari Ikulu jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Tume ya Kutathmini na Kushauri kuhusu Maboresho ya Kodi nchini, Balozi Ombeni Sefue, amesema kuwa kiwango cha sasa cha pato la taifa ni asilimia 12.1, ambacho hakikidhi mahitaji ya kimataifa kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi.
“Tuna kazi kubwa ya kuongeza mapato ya serikali ili kufikia lengo hilo,” alisema Balozi Sefue.
Balozi Sefue alisisitiza umuhimu wa kupanua wigo wa ulipaji kodi, kuziba mianya ya ukwepaji kodi, na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.
“Tunahitaji kuunda mazingira mazuri ya ukusanyaji wa kodi,” aliongeza.
Aidha, alisisitiza kuwa ukuaji wa uchumi unaweza kuimarishwa pia kupitia uzalishaji, uwekezaji, na biashara, kuongeza uwezo wa mwananchi mmoja mmoja kwa njia ya matumizi, akiba, na uwekezaji.
“Tunahitaji kujenga uelewa wa pamoja ili kuimarisha uzalendo na ushiriki wa wananchi na wadau katika kutengeneza mapendekezo yatakayosaidia taifa,” alisema Balozi Sefue.
Zoezi la ukusanyaji wa mapendekezo ya wadau kuhusu maboresho ya mfumo wa kodi linatarajiwa kuchukua miezi mitatu, na baadaye mapendekezo hayo kuwasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa ajili ya utekelezaji.