Serikali: Tumejipanga Stars kung’ara Afcon 2027

DODOMA; Serikali imesema imejipanga kuhakikisha timu ya soka ya Taifa ‘Taifa Stars’ haishiriki tu, bali inashindana kwa kiwango cha juu fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027 zitakazofanyika hapa nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Hassan Kungu aliyetaka kujua mkakati wa Serikali kuandaa Taifa Stars madhubuti itakayowakilisha Taifa katika fainali hizo.
Amesema serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF) imeweka mikakati ya muda mfupi, wa kati na ya muda mrefu kwa ajili ya maandalizi ya timu ya Taifa.
“Serikali inatambua kuwa uenyeji wa fainali za Afrika (AFCON) mwaka 2025 ni heshima kubwa na fursa ya kihistoria. Hivyo, tumejipanga kuhakikisha timu yetu haishiriki tu, bali inashindana kwa kiwango cha juu,” amesema Naibu Waziri.