Serikali wekezeni katika sekta ya habari

DAR-ES-SALAAM: MKUU wa Shule ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Mona Mwakalinga amesisitiza umuhimu wa serikali kuwekeza zaidi katika sekta ya habari na mawasiliano.

Akizungumza na mwandishi wa Daily News Digital katika mahojiano maalum, Dk. Mona alitaja umuhimu wa kuboresha sera na sheria za habari ili kukidhi mahitaji ya ukuaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) nchini.

Dk. Mona alibainisha kuwa sekta ya habari inakua kwa kasi na inahitaji uwekezaji mkubwa katika mafunzo na vifaa ili kuandaa wataalamu watakaokuwa na uwezo wa kuleta mabadiliko  katika tasnia ya habari..

Advertisement

“Kuwekeza katika watu na vifaa ni muhimu na tunahitaji wataalamu  wengi watakaoweza kubadilisha tasnia ya habari,” alisema.

Aliongeza kuwa ukuaji wa mitandao ya kijamii umeleta changamoto katika uwasilishaji wa taarifa, ambapo wadau wengi wanashindwa kufuata maadili ya taaluma ya habari, hivyo kusababisha upotoshaji wa taarifa na udhalilishaji wa watu mitandaoni.

“Ni muhimu kufuata maadili ya habari na kutoa taarifa sahihi mitandaoni kwa kuzingatia maadili ya taaluma sio kuandika taarifa ambazo hazina tija kwa jamii  tufike mahali tulinde wenzetu na tujilinde na sisi,” alisisitiza.

Dk. Mona pia alihimiza wanafunzi wa vyuo vikuu, hususan wanawake, kuzingatia masomo na kujiepusha na vishawishi vinavyoweza kuathiri ndoto zao.

“Kujiamini ni muhimu.wasikubali  vishawishi vya dunia vinavyochangia kusitisha ndoto na malengo ya wasichana wengi vyuoni,” alimalizia.

SOMA: Majaliwa atoa maagizo kwa Mamlaka Sekta ya Habari

Dk. Mona ni mhadhiri wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akiwa na uzoefu mkubwa katika sanaa za filamu, ambapo amekuwa akitumia sanaa hizo kuwasilisha maudhui mbalimbali kwa jamii.