Serikali ya ADC kulinda diplomasia ya Tanzania

DODOMA : CHAMA cha Alliance for Democratic Change (ADC) kimesema serikali yake italinda uhusiano wa Tanzania na nchi nyingine. Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho 2025-2030 imeeleza serikali hiyo itastawisha uhusiano huo na kuutumia kwa faida za kimaendeleo hasa ya kiuchumi na kijamii kwa manufaa ya Tanzania.

“Diplomasia ya uchumi katika mahusiano itakuwa ni miongoni mwa silaha za kuchochea maendeleo ya taifa letu katika nyanja za kibiashara, kielimu, kubadilishana uzoefu, utaalamu na kukuza mahusiano baina ya Serikali ya ADC na mataifa mengine,” imeeleza ilani.

Imeongeza: “Ushirikiano wa kikanda katika masuala ya usalama, uchumi, biashara, miundombinu pia utapewa kipaumbele kutoka ndani na nje ya Afrika kwa ujumla”.

Ilani imeeleza Serikali ya ADC itahakikisha masilahi na fursa za kimaendeleo kwanza zınatengwa kwa wananchi wa Tanzania na ikibidi kumpa mgeni fursa hizo ni lazima ashirikiane na serikali au wenyeji wa eneo ambako fursa ya uwekezaji inapatikana.

“Serikali ya ADC itaweka idara maalumu ya kuangalia masilahi ya nchi na watu wake katika mambo yanayoshirikisha wageni, ikıwa ni sambamba na kuwashauri wananchi juu ya mahusiano sahihi na yenye tija katika kushirikiana na wageni,” imeeleza ilani.

ADC imeahidi kuruhusu kuwepo kwa ofisi za ushauri na uwakala kwa wananchi kuhusu ushirikiano kutokana na rasilimali zao ili kuwasaidia hata katika uwekezaji wa ndani baina ya Watanzania wenyewe kwa wenyewe. SOMA : ADC yaja na mikopo kwa wanaume, afya, elimu bure

Chama hicho kimeahidi kuwa na viongozi wazalendo, wawajibikaji, waadilifu, waaminifu, wabunifu, wenye nidhamu, upendo, huruma, utu, upole, ukarimu, wenye heshima kwa watu, watakaoongozwa na hekima na busara na wenye mapenzi na nchi yao.

“Serikali itakayoongozwa na ADC itaweka misingi na sheria madhubuti juu ya masuala ya kujitolea katika ujenzi wa faifa letu, wananchi watapatiwa fursa mbalimbali na tuzo kama ni ujira au heshima kwa walichokifanyia nchi yao kwa kujitolea,” imeeleza ilani.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button