NAIBU Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi, Juma Makungu Juma, ametoa muda wa siku saba, ili kuvunjwa kwa nyumba iliopo Fuoni Migombani, kwa madai msimamizi wa nyumba hiyo, Hafidh Ahmed Mohammed, amejenga kinyume na utaratibu wa kisheria za mipango miji na vijiji.
Ametoa agizo hilo baada ya kufanya ziara katika eneo hilo la Fuoni Jitimai Shehia ya Migombani Wilaya ya Magharibi B na kumuagiza msimamizi kusimamisha ujenzi, ikiwa ni pamoja na kuvunja eneo ambalo alilazimika kuweka njia na badala yake kwenda kinyume na taratibu zilizopo.
Amesema serikali haina malengo ya kumdhulumu mwananchi, ila ni vyema kwa wananchi kutambua umuhimu wa kuweka njia wakati wanapofanya ujenzi, hivyo kutokana na kitendo kilichofanywa na mmiliki huyo, serikali inalazimika kuchukua hatua.
“Tunapofanya taratibu za ujenzi kwanza tunapaswa kujua, hatupaswi kuziba njia ambayo inatumiwa na jamii, kufanya hivyo ni kosa na yoyote atakayekua anakiuka taratibu za ujenzi hatua huchukuliwa dhidi yake,” amesema.
Amewataka viongozi kushirikiana pamoja katika kutatua migogoro ya ardhi nchini, ambapo mzozo huo haukupaswa kutokea, endapo viongozi waliopewa dhamana ya utoaji vibali wangetimiza wajibu wao kikamilifu.
Ameeleza kuwa kwa mujibu wa sheria anayepaswa kutoa vibali vya ujenzi, ni Kamati ya Udhibiti na Usimamizi Vibali vya Ujenzi (DCU), ambayo mwenyekiti wake ni Mkurugenzi Mipango Miji na Vijii, hivyo wananchi wanapotaka kujenga ni vyema kufika katika taasisi hiyo iliyowekwa kisheria.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mipango Miji na Vijiji Kutoka Kamisheni ya Ardhi, Muchi Juma Ameir aliwataka wananchi wanapotaka vibali vya ujenzi kufika sehemu husika iliyowekwa kisheria, ili kuepuka athari, ambayo inaweza kutokea.