DAR ES SALAAM; SERIKALI imesema itaendelea kuwalea wazalishaji wawekezaji na wazalishaji wa ndani ya nchi, ili waweze kukuza mitaji yao na kuchangia katika maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk Hashil Abdallah, wakati wa ziara yake kwenye kiwanda cha Kairuki Pharmaceutical Limited kilichopo Kibaha mkoani Pwani .
Akiongoza ujumbe wa Makatibu Wakuu, wakiwemo Dk Natu Mwamba (Wizara ya Fedha), Dk John Jingu (Wizara ya Afya), na Katibu Tawala Mkoa wa Pwani, Rashid Mchatta, Dk Abdallah ameeleza kuwa lengo la ziara hiyo lilikuwa kujionea shughuli za uzalishaji, kusikiliza changamoto zinazokikabili kiwanda hicho na kutafuta suluhisho.
Dk Abdallah pia amebainisha kuwa ziara hiyo inaashiria dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuimarisha sekta ya viwanda nchini kwa kuwaunga mkono wawekezaji wa ndani na kuwawezesha kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Dk Abdallah akiwa na ujumbe huo amekipongeza kiwanda hicho kwa utendaji kazi mzuri na kuahidi ushirikiano kutoka kwa wizara husika katika kutatua changamoto zilizopo ili kuwezesha kiwanda hicho kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Pia amebainisha kuwa kiwanda hicho kinachotoa ajira za moja kwa moja 200 na zisizo za moja kwa moja 300 ni moja ya viwanda vya kimkakati vinavyozalisha dawa za maji tiba mbalimbali nchini ili kupunguza utegemezi wa kuagiza dawa hizo nje ya nchi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda hicho, Dk Muganyizi Kairuki akitoa taarifa kwa ujumbe huo amesema kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha chupa za maji tiba milioni 50 kwa mwaka, ambapo asilimia 60 huuzwa nchini wakati asilimia 40 huuzwa nchi za nje zikiwemo Rwanda, Comorro, Malawi, Zambia, Namibia, Congo, Msumbiji na Yemen.