SERIKALI kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), imefanya upimaji wa udongo na usanifu uliokamilika kwa ajili ya kujenga daraja la kudumu katika mto Mngeta barabara ya Mchombe- Lukorongo- Ijika katika Halmashauri ya Mlimba , wilayani Kilombero, mkoani Morogoro .
Meneja wa Tarura Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, Sadiki Karume alisema tayari hatua za muda mfupi na mrefu zimechukuliwa za kuboresha mundombinu na kujenga daraja imara na la kudumu la kuviunganisha vijiji sita za kata ya Mchombe.
“ Tayari hatua hii imechukuliwa na Tarura Makao makuu ya kujenga daraja la kudumu ambao ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu akiwa ziarani katika Hamashauri ya Mlimba wilayani Kilombero” alisema Mhandisi Karume
Karume alisema daraja la Mbassa linaunganisha vijiji vya Isago, Lukolongo, Mchombe na Ijia.
Karume alisema kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha Mto Mbassa umejaa maji kwa kiwango kikubwa na hivyo kumesababisha daraja lililikuwepo la mbao kusombwa na mafuriko na hiyo imesababisha kukatika kabisa kwa mawasiliano kati ya vijiji husika.
“Kwa sasa mto Mngeta umejaa sana maji na yanaenda kwa kasi,hivyo basi kazi zitaanza punde maji yatakapopungua mtoni kwa kuwa vifaa vyote vya ujenzi vipo tayari” alisema Mhandisi Karume
Hivi karibuni wananchi wa kutoka katika vijiji hivyo sita aliiomba serikali kuwajengea daraja la kudumu la mto Mbassa baada ya daraja la mbao kusombwa na maji Aprili 11, mwaka huu na kuleta adha kubwa kwao kushindwa kuvuka kutoka upande mmoja kwenda mwingine .
Diwani wa Kata ya Mchombe , Batholomeo Swalla alimwomba Rais Dk Samia Suluhu Hassan kusaidia uwezeshaji wa kupatikana daraja la chuma litakalokuwa imara litakalodumu kwa muda mrefu na kuwa ni mkombozi wa kuviunganisha vijiji vyao .
Kwa mujibu wa Diwani huyo kuwa zaidi ya watu 1,000 wanavuka kila siku kwenye daraja hilo kabla ya kusombwa na maji na kumeathiri shughuli za kijamii na kimaendeleo.