SERIKALI imesema shughuli za uchumi nchini zimeendelea kuimarika licha ya changamoto zinazoikabili kutokana na utekelezaji wa Sera za ya Fedha ya kupunguza ukwasi katika nchi zinazoendelea
Ikiwemo pia migogoro ya kikanda na kimataifa, kuongezeka kwa bei ya petrol, gharama kubwa za mikopo na mabadiliko ya tabianchi.
Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amesema hayo Novembe 7,2024 wakati akifungua Kongamano kati ya Wizara na Wahariri wa Vyombo vya Habari mkoani Morogoro.
Hotuba ya Dk Nchemba ilisomwa kwa niaba yake na Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA Leonard Mkude .
Dk Nchemba amesema pamoja na changamoto hizo pato halisi la Taifa lilikuwa kwa wastani wa asilimia 5.1 mwaka 2023 likilinganishwa na asilimia 4. 7 mwaka 2022 ambapo ukuaji huo ulichangiwa kwa kiasi kikubwa, kilimo, ujenzi na uchimbaji madini.
Waziri alitaja viashiria vya uchumi kwa nusu ya mwaka 2024 vinaonesha uchumi kuendelea kuimarika kutokana na jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na serikali ya awamu ya sita za kuboresha mazingira ya uwekezaji,biashara na kuimarisha sekta uzalishaji na huduma za jamii.
Amesema kufuatia jitihada hizo, pato halisi la taifa kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2024 lilikuwa kwa wastani kwa asilimia 5.4 ukilinganisha na asilimia 4.8 katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2023.
Waziri Dk Nchemba amesema pato la taifa linatarajia kukuwa kwa wastani wa asilimia 5.8 mwaka 2025 na asilimi 6.1 mwaka 2026
“ Ukuaji huu utategemea utekelezaji endelevu wa miradi ya kimikakati inayohusisha miundombinu ya nishati na usafirishaji,kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi,jitihada za serikali katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara,”amesema Dk Nchemba
Dk Nchemba amesema ukuaji huo utategemea utekelezaji wa program ya kuendeleza sekta ya kilimo awamu ya pili –ASDP II, utekelezaji wa mapendekezo na mkakati wa Tume wa haki jinai, uwepo wa Utawala bora pamoja na uwekezaji wa serikali katika sekta za huduma za jamii.
Waziri amesema Serikali pia lifanikiwa kudhibiti mfumuko wa bei ambao ulikuwa asilimia 3.2 mwaka 2023/24 ,kiwango ambacho kipo ndani ya lengo la nchi kati ya asilimia tatu hadi asilimia tano sawa na mchangomano wa kiuchumi kikanda kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na SADC.
Waziri amesema kiwango hicho kilikuwa chini ya asilimia 4.7 ya mwaka 2022/23 na kwamba kupungua huko kunatokana na sera madhubuti ya fedha na bajeti, kuimarika kwa bei ya baadhi ya bidhaa zilizoagizwa kutoka nje ya nchi na utoshelevu wa chakula nchini.
Dk Nchemba amesema mfumuko wa bei nchini unatarajiwa kubaki ndani ya lengo la nchi la asilimia 3 hadi 5, ukichagizwa na matarajio ya upatikanaji wa chakula cha kutosha nchini, kuimarika kwa upatikanaji wa umeme ,utulivu wa bei za bidhaa katika soko la dunia na utekelezaji wa sera madhubuti za fedha na bajeti.