KATIKA Kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa Ebola nchini, serikali imeweka maabara tembezi ya kupima virusi vya ugonjwa huo ambayo imefungwa katika kituo cha afya Kabyaire kilichopo wilaya ya Misenyi mkoani Kagera.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Dk Issessanda Kaniki akizungumza leo Jumamosi, Septemba Mosi, 2022 katika kikao cha wadau wa afya dhidi ya mlipuko wa Ebola amesema mashine hiyo ina uwezo wa kutoa majibu ndani ya saa mbili na tayari jopo la wataalamu wameshawasili kituoni hapo.
Aidha, amesema mkoa umetenga hospitali 12 ambazo zitakuwa zinatoa matibabu ya Ebola kwa atakayegundulika.
“Mkoa umetenga pia maeneo maalum kwa ajili ya kuweka wagonjwa wa Ebola vituo vyote vya afya mkoani hapa baada ya kuwapima na kuonekana na dalili litakuwepo gari la wagonjwa kwa ajili ya kuwasafirisha kwenye vituo maalum,” amesema.
Mtaalam huyo ameongeza kuwa kila Halmashauri imetenga eneo la karantini kwa ajili ya kuwaweka watu wnaohisiwa kuwa na dalili za ugonjwa huo hatari na endapo kuna watakaobainika na ebola, matibabu yataanza mara moja.
Amesema Mkoa wa Kagera umechukua tahadhari zote kutokana na eneo hilo kukaribiana na nchi kadhaa zikiwemo Burundi, Rwanda, Uganda, Sudan ya Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Amesema tahadhari nyingine ni kutoa elimu mipakani ili wananchi wapate uelewa juu ya ugonjwa wa Ebola namna ya kujikinga na kutoa taarifa haraka.
Naye Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma, Dk Amma Kasangala amesema, haiwezekani kufunga mpaka kwa kuwa kuna shughuli mbalimbali zinaendelea za uzalishaji kwa wananchi badala yake watajikita katika kutoa elimu ya jinsi ya kujikinga na virusi hivyo kwa kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka, kutumia vitakasa mikono, kutosogeleana na kugusana na kuepuka kusafiri safari zisizo za lazima katika nchi zenye wagonjwa wa Ebola.
Philbert Johansen mkazi wa manispaa ya Bukoba amesema tayari wakazi wa hapa wameanza kuchukua tahadahari dhidi ya Ebola kwa kuweka ndoo za maji safi na sabuni maeneo ya biashara zao.
Hivi karibuni, nchi ya Uganda iliripoti kisa cha ebola ambapo hadi sasa watu kadhaa wameshafariki na wengine wanapata matibabu.
Tanzania inachukua kila aina ya tahadhari baada ya kuripotiwa ugonjwa huo kwani upande wa Kaskazini Magharibi inapakana na Uganda huku muingiliano wa wananchi baina ya mataifa hayo ukiwa mkubwa.