Serikali yajizatiti utafiti, umwagiliaji kuinua kilimo

NANENANE ni Sikukuu ya Wakulima nchini. Inahusisha pia sekta ya ufugaji na uvuvi ikiwa na hadhi ya Maonesho ya Kimataifa ya Nanenane.

Awali, sikukuu hii ilijulikana kama Sabasaba ikiadhimishwa Julai 7 kwa ajili ya wakulima na wafanyabiashara lakini baadaye ilihamishiwa Agosti 8 na Julai 7 kubaki maonesho ya kibiashara.

Sikukuu hii hufanyika kitaifa kwa mzunguko wa kikanda katika kanda saba ambazo ni Mashariki (Dar es Salaam, Pwani, Tanga na Morogoro); Magharibi (Kigoma na Tabora); Kanda ya Kaskazini (Manyara, Arusha na Kilimanjaro); na Kanda ya Ziwa Mashariki (Shinyanga, Mara na Simiyu).

Advertisement

Nyingine ni Kusini (Mtwara na Lindi); Nyanda za Juu Kusini (Mbeya, Iringa, Njombe, Songwe, Rukwa, Katavi na Ruvuma); na Kanda ya Ziwa Magharibi (Mwanza, Geita na Kagera). Mwaka jana serikali iliamua maadhimisho hayo yawe ya kimataifa, na kitaifa yafanyike katika eneo moja ambalo walichagua Mkoa wa Mbeya katika Uwanja wa John Mwakangale.

Agosti Mosi, mwaka huu, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alifungua maonesho hayo jijini Mbeya ambapo kabla ya ufunguzi alipita katika mabanda kujionea teknolojia zilizopo. Katika hotuba yake alisema katika utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (2020-2025), serikali imedhamiria kuendeleza sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kuongeza uzalishaji, tija na thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi pamoja na kukuza kipato na kuongeza ajira kwa wananchi.

“Kwa sababu hiyo serikali imeongeza bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutoka shilingi bilioni 275 mwaka 2021/2022 hadi shilingi bilioni 295 mwaka 2023/24 na Wizara ya Kilimo kutoka shilingi bilioni 294 kwa mwaka 2021/2022 hadi shilingi bilioni 970 mwaka 2023/2024,” anasema.

Dk Mpango anasema ongezeko hilo linalenga kuimarisha utafiti na huduma za ugani, kutoa ruzuku za pembejeo za kilimo, mifugo na uvuvi.

Aliagiza elimu ya afya ya udongo ifike kwa watu wote kupunguza upotevu wa mbolea unaotumiwa kiholela na wakulima. “Kwanza mtu ajue eneo alipo afya yake ya udongo iko hivi, vinginevyo tunapoteza kiasi kikubwa sana cha mbolea ambazo zingeweza kutumika sehemu nyingine kwa kuwa zinatumika bila kujua uhitaji wa eneo husika,” anasema Dk Mpango.

Alieleza hayo akiwa katika banda la Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) ambako Mkurugenzi wa Tari, Dk Geofrey Mkamilo alimueleza Dk Mpango kuwa ramani zilizopo zinaonesha afya ya udongo kwa nchi nzima. “Lakini kwa kutaka undani udongo ule una nini, unapunguka kitu gani, unachukua sampuli ili upimwe na mkulima kupewa ushauri nini afanye,” alisema Dk Mkamilo.

Katika hatua nyingine Dk Mpango alitaka kujua kwanini uzalishaji wa mbegu nchini ni changamoto ambapo Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alieleza miundombinu ya umwagiliaji ndio tatizo lakini mpangowa ujenzi wake unaendelea katika vituo vya utafiti nchini.

“Mwaka huu tumeanza kujenga miundombinu ya umwagiliaji ili vituo vya utafiti vizalishe mbegu kwa wingi nchi nzima,” alisema Bashe na kufafanua kuwa mwanzoni serikali ilizalisha mbegu lakini kutokana na kutotosheleza hivi sasa inashirikiana na sekta binafsi 29. Kuhusu mbolea, Dk Mpango ameagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), kusimamia wakulima wapate mbolea kwa wakati kuondoa manung’uniko ya ucheleweshaji wa mbolea ya ruzuku aliyoyakuta kwa wakulima wanawake mkoani Ruvuma. “Nataka hilo liishe. Msimu wa mvua mbolea iwepo. Hili mlisimamie wakulima wapate mbolea ya kutosha na kwa wakati,” aliagiza.

Mkurugenzi Mtendaji TFRA, Dk Stephano Ngairo anasema amepokea agizo hilo na tayari wameongeza mtandao wa usambazaji wa mbolea kwa wakulima pamoja na idadi ya mawakala. Alipotembelea Wakala wa Mbegu Tanzania (ASA), Dk Mpango alieleza ustawi wa nchi unategemea utafiti.

“Lazima tufanye utafiti, tusipofanya hivi tutakwisha ili kama ni mbegu ziwepo za kwetu. Hao wanaotuletea mbegu mazingira yao na yetu ni tofauti.”

Naye Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Agosti 3 alitembelea maonesho hayo na kujionea shughuli za kibunifu na kitafiti kutoka kwa watafiti. Akiwa katika Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Majaliwa alisema amemwalika mwekezaji kutoka nchini Urusi kwa ajili ya kuwekeza kwenye mitambo ya kukaushia matunda.

“Yeye ana mitambo ya kukausha haya mazao yetu ambayo huwa yanaharibika kwa kuoza kama nyanya, zabibu, ndizi na mazao mbalimbali yanayoharibika ili yasiharibike,” anasema.

Majaliwa aliyasema hayo baada ya kuona teknolojia ya kukausha zabibu iliyofadhiliwa na tume hiyo na kuelezwa kuwa Costech imetoa Sh milioni 400 kwa Tari, Kituo cha Makutupora Dodoma kwa ajili ya kutengeneza mitambo ya kuongeza thamani kwenye zabibu.

Amesema mitambo hiyo pia itasaidia kukausha maembe, machungwa na mengine ambayo yatauzwa kwa thamani kubwa. Ofisa Mwandamizi wa Uratibu wa Utafiti kutoka Costech, Dk Deogracious Protas amemweleza Majaliwa kuwa kiasi hicho cha fedha kimetengeneza maabara ya kisasa ya kuwasaidia wakulima.

Maonesho ya mwaka huu yametumika pia kuwahamasisha wadau wa sekta za mifugo na uvuvi kujisajili kushiriki vyema katika Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika 2023 (AGRF) ili wafungue fursa za kibiashara ndani na nje ya nchi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alisema wizara inafanya jitihada za kuhamasisha wadau wa sekta za mifugo na uvuvi kushiriki katika mkutano huo utakaofanyika kuanzia Septemba 5-8, mwaka huu kupata fursa za kiuchumi na kuongeza wigo wa mawasiliano ya kibiashara wa ndani na nje ya nchi.

Jukwaa hilo litachochea ufanisi zaidi wa programu ya kielelezo ya “Jenga Kesho Iliyo Bora” inayowezesha vijana kupata elimu ya vitendo ya unenepeshaji wa mifugo na viumbe vya kwenye maji inayofanyika kutokana na maono na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ambapo hadi sasa vijana 240 wapo kwenye mafunzo hayo.

Amesema matumaini ni kwamba “Jenga Kesho Iliyo Bora” itashuka ngazi ya mkoa na wilaya zijiendeshe pamoja na kuongeza kundi la vijana kutoka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili wapate pia mafunzo hayo. Kuelekea uchumi wa buluu, Ulega anasema serikali itawezesha wavuvi wadogowadogo kuingia kwenye maji marefu wafanye shughuli za uvuvi na watakopeshwa boti bila riba, kunenepesha jongoo bahari na kilimo cha mwani.

4 comments

Comments are closed.