Serikali yashauriwa uwazi kudhibiti ubadhirifu

SERIKALI imeshauriwa kuweka wazi ripoti za mapato na matumizi ya miradi yake kwa ngazi mbalimbali ili kudhibiti wizi na ubadhirifu wa fedha umma.

Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Padre Dk Charles Kitima alisema ili taifa likabiliane na vitendo vya ubadhirifu wa fedha za umma linahitaji kujenga uadilifu.

Dk Kitima alisema serikali inapaswa kuweka wazi taarifa za mapato na kazi inazozifanya zinazogusa maisha ya watu kwa kuwa jambo hilo litawezesha wananchi kupima na kuiwajibisha serikali na si wabadhirifu pekee.

Mchambuzi wa masuala ya uchumi na biashara, David Kafulila, alisema vita dhidi ya rushwa na ufisadi siku ni endelevu na hakuna nchi duniani iliyomaliza rushwa.

Kafulila alisema ili kudhibiti ubadhirifu wa fedha za umma njia ya uhakika ni kuongeza uwazi katika mapato na matumizi katika utekelezaji wa miradi ili kuongeza wigo wa wananchi na jumuiya za kiraia kusimamia uwajibikaji wa serikali.

“Bunge, mabaraza ya madiwani na mamlaka za uchunguzi zinazomsaidia rais ni sehemu moja, lakini uimara wa vyombo vya habari na jumuiya za kiraia ni msingi pia katika kushiriki ujenzi wa uwajibikaji,”alisema Kafulila

Alisema Ripoti ya Transparency International ya January 25 mwaka huu inaonesha kiwango cha rushwa hapa nchini kupungua kutoka nafasi ya 94 mpaka 87 kati ya nchi 180 zilizofanyiwa tathimini kwa vigezo 180.

Kafulila alisema ripoti hiyo ya mwaka ni tathimini ya mwaka jana ambao kwa sehemu kubwa ni awamu ya sita na ripoti ya mwaka jana ni tathimini ya mwaka juzi ambayo ni awamu ya tano, hivyo inaonesha Taifa kupiga hatua japo sio kubwa.

Katibu Mkuu wa Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira (TRAMEPRO), Bonaventura Mwalongo, alisema ni kweli wimbi la ubadhirifu wa fedha za umma lipo na kusababisha malalamiko kwa wananchi.

Ili kudhibiti vitendo hivyo, alisema kuna haja ya kuongezeka kwa uwazi katika shughuli za serikali kwa kuwa mahali ambapo kuna usiri vitu vingi vinafichwa na viovu pia hupata fursa ya kufichwa.

“Panapokuwepo uwazi na elimu ikatolewa kwa umma kama ambvyo gazeti hili la serikali linavyofanya, itasaidia kujua nafasi ya wananchi katika usimamizi wa rasilimali zao na kuhoji pale mambo yanapokuwa hayaendi sawa, hii itasaidia kutia hofu kwamba wananchi wako macho dhidi ya rasilimali zao,”alisema Mwalongo

Alisema baadhi ya watu hushiriki vitendo vya ubadhirifu wa fedha na mali za umma kwa lengo la kutaka kuhujumu jitihada na dhamira ya kiongozi mkuu wa nchi na serikali kwa ujumla lakini pia ni ubinafsi wa baadhi ya watu wa kutaka kujilimbikizia mali kwa kukosa uzalendo na kuwanyonya masikini kwa kujipatia mali zisizohalali.

Alisema jambo hilo linaathiri uchumi, amani ya nchi kwa kuwa manung’uniko yapozidi yanaweza kuibua matatizo zikiwemo vurugu, wizi na ujambazi katika jamii pamoja na kudidimiza juhudi za kujikomboa na kujitegemea kama nchi.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x