TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) inachunguza ujenzi wa kituo cha afya cha kata ya Ushirika wilayani Mbogwe mkoani Geita kufuatia mradi huo kudaiwa kusuasua na kutokamilika kama ulivyopangwa.
Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Afya Ushirika ulianza Oktoba 11, 2022 baada ya kupokea Sh milioni 500 kutoka serikali kuu kupitia fedha za tozo za miamala ya simu.
Akisoma taarifa ya mradi huo mbele ya Waziri wa Madini Anthony Mavunde alipofika kukagua mradi huo, Mtendaji wa Kata ya Ushirika, Juma Luchagula amesema Sh milioni 63.1 zinahitajika kukamilisha mradi huo.
Amesema mradi unahusisha jengo la wagonjwa wa nje, jengo la wodi ya wazazi, jengo la upasuaji, jengo la kufulia, jengo la maabara, njia ya kutembelea na kichomea taka.
Amesema katika utekelezaji wa mradi, serikali imechangia Sh milioni 500, halmashauri Sh milioni 60, nguvu ya wananchi Sh milioni 15, Mfuko wa Huduma Endelevu za Maji na Mazingira (WASH) Sh milioni 23 na hivo jumla ni Sh 598.
Mkuu wa mkoa wa Geita Martine Shigella amesema uchunguzi umekuja kufuatia uwepo wa viashiria vya ufujaji wa fedha za mradi huo na kusababisha mradi kutokamilika kama ulivyopangwa kwa sababu za usimamizi dhaifu.
SOMA: Wanaochezea mapato ya serikali kuchukuliwa hatua
“Mtendaji wa kijiji, mtendaji wa kata na kamati zao hawakutimiza wajibu wao ipasavyo, sasa kwa sababu serikali tuna utaratibu wetu jambo hili tumeshalipeleka Takukuru, na Takukuru tayari imeshaanza kuchukua hatua
“Kwa hiyo wanakamilisha taratibu zote, wale wanaopaswa kuchukuliwa hatua za kinidhamu wapelekwe kwenye nidhamu, na wale wanaohusika kwenye taratibu za kimahakama tutaendelea na mahakama,” amesema.
Mbunge wa Jimbo la Mbogwe, Nicodemus Maganga amekiri mradi huo umekwama kukamilika kwa bajeti ya awali na hivo kuhitajika bajeti nyingine huku akitaka hatua zichukuliwe kuleta nidhamu kwa watumishi.
“Sisi kwenye baraza la madiwani kwa kweli tuligoma kupitisha zile milioni 60 kwa sababu milioni 500 zilikuwa zinatosha kumaliza kituo lakinu tunashukuru Takukuru walichukua hatua,” amesema Maganga.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoni Geita, Nicolous Kasendamila amekemea tabia ya baadhi ya viongozi kutumia mwamvuli wa kisiasa kukwamisha miradi ya maendeleo.
Naye Waziri Mavunde ametoa wiki moja kwa halmashauri ya wilaya ya Mbogwe kutangaza tenda ya ukamilishaji wa kituo cha afya Ushirika na Takukuru iongeze kasi ya uchunguzi wa mapungufu ya mradi huo.
Mavunde amekiri kubaini kasoro kwenye mradi huo kwani fedha ya serikali haijatendewa haki na hivo malekezo ya serikali lazima yasimamiwe na yafanyiwe kazi kwa haraka.